Mshukiwa wa biashara ya ulanguzi wa binadamu akamatwa Nairobi

Muhtasari

•Habeta amehusishwa na takriban operesheni nne za ulanguzi wa binadamu ambapo makundi ya raia wa Eritrea waliingizwa Ulaya kinyemela kupitia Asia.

Image: TWITTER// DCI

Raia mmoja wa Uholanzi ambaye amekuwa mafichoni kwa kipindi cha miaka minne baada ya kuhusishwa na biashara ya ulanguzi wa binadamu ametiwa gerezani baada ya kukamatwa hapa nchini Kenya.

John Habeta 53, ambaye ana asili ya Eritrea alikamatwa jijini Nairobi na maafisa wa DCI baada ya INTERPOL kutoa notisi ya kukamatwa kwake.

Maafisa wa DCI wamesema Habeta anaaminika kuwa kiongozi wa shirika la kimataifa la ulanguzi wa binadamu linalofanya kazi kisiri.

Habeta amehusishwa na takriban operesheni nne za ulanguzi wa binadamu ambapo makundi ya raia wa Eritrea waliingizwa Ulaya kinyemela kupitia Asia.

Mshukiwa alipokamatwa alikabidhiwa mikononi mwa mamlaka ya Uholanzi baada ya waziri wa masuala ya ndani Fred Matiang'i kutangaza alitangaza kuwepo kwake nchini kama kinyume na maslahi ya taifa.

Habeta ataendelea kuzuiliwa huko Uholanzi ambako baadae atafunguliwa mashtaka.