Mwanamke ajiteketeza pamoja na wanawe wawili baada ya mumewe kutoka nje ya ndoa Kakamega

Muhtasari

•Vuyanzi na mumewe walikuwa wameoana kwa miaka 12 na walikuwa na watoto watatu wenye umri wa miaka 11, 4 na 2.

•Mtoto wake wa tatu alinusurika kwenye mkasa huo baada ya kuruka nje ya nyumba kupitia dirisha.

Helen Vuyanzi akiwa na watoto wake watatu. Alijiteketeza hadi kufa pamoja na wawili aliowashikilia
Helen Vuyanzi akiwa na watoto wake watatu. Alijiteketeza hadi kufa pamoja na wawili aliowashikilia
Image: HILTON OTENYO

Mwanamke mmoja alijiteketeza kwa moto pamoja na watoto wake wawili mnamo sikukuu ya mwaka mpya katika kijijii cha Sirende, kaunti ndogo ya Lugari baada ya kuzozana na mumewe. 

Mtoto wake wa tatu alinusurika kwenye mkasa huo baada ya kuruka nje ya nyumba kupitia dirisha.

Hellen Vuyanzi, 35 aliripotiwa kuzua ugomvi na mumewe siku ya Jumamosi kisha wakachukuliwa na maafisa wa polisi wakiongozwa na kamanda wa Lugari Bernard Ngungu na kupatiwa ushauri.

Vuyanzi alirudi nyumbani lakini mumewe hakurejea ili kuepusha msuguano zaidi.

Bosi wa polisi alisema  marehemu alikuwa amemshutumu mumewe kucheza karata nje ya ndoa baada ya kugundua kwamba alikuwa akichumbiana na mwanamke mwingine.

Ngungu alisema mwanamke huyo huenda alinunua petroli na kuificha ndani ya nyumba kabla ya kuzua ugomvi na mumewe.

Jirani mmoja ambaye hakutaka  kutajwa jina alisema wanandoa hao wamekuwa na mzozo usioisha tangu mwanamke huyo alipoanza kumshuku mumewe.

“Wamekuwa wakizozana kwa madai ya kutokuwa mwaminifu lakini hatukutarajia yangeisha hivi,” alisema.

Vuyanzi na mumewe walikuwa wameoana kwa miaka 12 na walikuwa na watoto watatu wenye umri wa miaka 11, 4 na 2.

Helen Vuyanzi, 35, akiwa na mtoto wake mdogo wa kiume
Helen Vuyanzi, 35, akiwa na mtoto wake mdogo wa kiume
Image: HILTON OTENYO

Stephens Okila, shemeji wa marehemu, alisema alikuwa mbali na nyumbani wakati kaka yake alipompigia simu na kumwarifu kwamba alifahamishwa kuwa nyumba yake inateketea.

"Tulikimbia huko na kudhibitisha kama ni kweli. Kwa bahati mbaya, mke wake na watoto wawili wenye umri wa miaka 4 na 2 walikufia ndani ya nyumba. Mwana wao mkubwa alifanikiwa kutoroka kupitia dirishani,” Okila alisema.

Okila alisema hana ufahamu kuhusu mzozo wowote kati ya nduguye na mkewake. "Ningesema kama kuna tatizo kati yao kwa sababu niko karibu na familia."

Andrew Otieno, alisema wanashuku shemeji yake alitangulia kuwapa watoto dawa za usingizi kabla ya kuchoma nyumba hiyo.

"Mwana mkubwa aliamka kutoka usingizini na akafanya juhudi kutoka nje ya nyumba iliyokuwa inateketea kabla ya kuwaarifu wanakijiji kuhusu tukio hilo," Otieno alisema.

Vuyanzi na watoto hao wawili tayari walikuwa wamekufa wakati majirani walifanikwa kuzima moto huo.

Otieno alidai huenda Vuyanzi alitumia gesi ya kupikia na godoro kuwasha moto.

Ngungu alisema uchunguzi umeanzishwa kuhusiana na kifo cha mwanamke huyo na watoto wake