Mshukiwa wa ubakaji apigwa risasi kwenye makalio baada ya kupinga kukamatwa Murang'a

Muhtasari

•Wakati mshukiwa alitoroka korokoroni mwaka jana alikuwa amezuiliwa kwa kuhusika katika ubakaji wa genge na alikuwa na kesi mbili zingine za ubakaji katika mahakama ya Kigumo.

•Baada ya mshukiwa kuonekana hana nia ya kukamatwa kwa amani afisa mmoja alichomoa bunduki yake na kumpiga risasi kwenye kitako chake  cha kushoto.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Murang'a wanamzuilia mshukiwa wa ubakaji ambaye alikuwa ametoroka kutoka kizuizini mnamo Juni 4, 2021.

Andrew Ngugi Wairimu ,20, almaarufu kama Makai alitiwa mbaroni mjini Maragua asubuhi ya Jumatatu baada ya kuwashirikisha polisi katika msako mkali.

Kitengo cha upelelezi wa Jinai kimesema wakati mshukiwa alitoroka korokoroni mwaka jana alikuwa amezuiliwa kwa kuhusika katika ubakaji wa genge na alikuwa na kesi mbili zingine za ubakaji katika mahakama ya Kigumo.

Ilani ya kukamatwa kwake ilitolewa baada ya kutoroka na imechukua takriban miezi saba polisi kupata taarifa kuhusu alikojificha mshukiwa.

Polisi walimvizia  katika eneo la mpakani la Maragua lakini mshukiwa ambaye alikuwa amejihami kwa panga akapinga kukamatwa na kujaribu kutoroka.

Baada ya mshukiwa kuonekana hana nia ya kuitikia kukamatwa kwa amani afisa mmoja alichomoa bunduki yake na kumpiga risasi kwenye kitako chake  cha kushoto.

Kufuatia hayo mshukiwa alikamatwa na kupelekwa katika hospitali ya Maragua ambako anaendelea kupokea  matibabu chini ya ulinzi mkali huku akisubiri kufikishwa mahakamani baada ya kuuguza jeraha.