Jamaa akiri kuua mpenziwe kinyama baada ya kusherehekea Krismasi pamoja

Muhtasari

•Shangazi ya Waweru ndiye aligundua mabaki ya mwili wa marehemu yakiwa yamefunikwa kwa blanketi wakati alipokuwa anapitia pale kumjulia mpwa wake hali na kumkabidhi pesa zake alizokuwa ametumiwa mama yake ambaye anaishi Marekani.

•Baada ya kukamatwa mshukiwa alikiri kumuua mpenzi wake na hata kupeleka wapelelezi mpaka mahali alipokuwa ameficha silaha alizotumia unyama huo.

•Inasemekana wawili hao walimiliki duka la kinyozi na urembo kabla ya mahusiano yao kupata doa.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika kaunti ya Kiambu wanazuilia jamaa mmoja mwenye umri wa miaka 25 anayeaminikia kuua mpenzi wake kinyama  mapema mwezi huu katika eneo la Thindigua kisha  kuacha mwili wake ukiozea ndani ya  nyumba yake na kuenda mafichoni.

Brian Waweru alikamatwa alasiri ya Jumatano baada ya mwili wa Everlyn Wanjiru ,24, kupatikana ndani ya nyumba yake  mnamo Jumanne jioni.

Shangazi ya Waweru ndiye aligundua mabaki ya mwili wa marehemu yakiwa yamefunikwa kwa blanketi wakati alipokuwa anapitia pale kumjulia mpwa wake hali na kumkabidhi pesa zake alizokuwa ametumiwa mama yake ambaye anaishi Marekani.

Maafisa wa DCI wamesem kwamba kwa wakati huo mshukiwa alikuwa ametoweka tayari. Wapelelezi walianzisha msako dhidi yake na kumkamata masaa kadhaa baadae katika eneo hilo la Thindigua.

Baada ya kukamatwa mshukiwa alikiri kumuua mpenzi wake na hata kupeleka wapelelezi mpaka mahali alipokuwa ameficha silaha alizotumia unyama huo.

Wapelelezi walibaini kwamba Waweru na Wanjiru hawajakuwa na uhusiano mzuri tangu mwezi Oktoba mwaka uliopita baada ya mshukiwa kumdhulumu marehemu na kukamatwa kufuatia hayo.

Wakati huo mshukiwa alifikishwa mbele ya mahakama ya Kiambu na kuachiliwa kwa dhamana.

Baba ya marehemu amesema familia ya Waweru ilikuwa imefanya majaribio kadhaa ya kusuluhisha kesi ile nje ya mahakama ila akakataa baada ya kugundua mshukiwa alikuwa na mazoea ya kutenda makosa.

Katika kipindi cha Krismasi mshukiwa alifanikiwa kushawishi mpenzi wake wapatane na wakajiburudisha pamoja hadi katika sherehe za mwaka mpya.

Jirani mmoja aliwaona wakiingia katika nyumba yao mnamo Januari 1 na hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho Everyln kuonekana akiwa hai.

Inasemekana wawili hao walimiliki duka la kinyozi na urembo kabla ya mahusiano yao kupata doa.

Kwa sasa mshukiwa amewekwa kizuizini akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji yanayomkabili