Tanzania: Kwanini Ndugai amejiuzulu? na historia ikoje?

Muhtasari

• Ingawa hii ni mara ya kwanza kwa Spika aliye madarakani kujiuzulu kwa hiyari yake katika historia ya Bunge la vyama vingi nchini Tanzania, uamuzi huu wa Ndugai ulikuwa ukitarajiwa na wengi kutokana na matukio yaliyotokea nchini katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Image: BUNGE/TANZANIA

Aliyekuwa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai (59), amejiuzulu wadhifa wake kupitia barua aliyoandika jana kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) - akiuelezea uamuzi huo kuwa umetokana na "uamuzi wake binafsi na uliozingatia na kujali maslahi mapana zaidi ya taifa, serikali na chama chake hicho".

Ingawa hii ni mara ya kwanza kwa Spika aliye madarakani kujiuzulu kwa hiyari yake katika historia ya Bunge la vyama vingi nchini Tanzania, uamuzi huu wa Ndugai ulikuwa ukitarajiwa na wengi kutokana na matukio yaliyotokea nchini katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Kauli yake aliyootoa mjini Dodoma takribani wiki moja iliyopita kuwa hatua ya Tanzania kukopa madeni makubwa katika taasisi za kimataifa inaweza kusababisha "nchi kuuzwa" iliibua mjadala mkali hadharani na sirini katika duru za mamlaka nchini - kauli yake ikitafsiriwa kama ni ukosoaji wa hatua ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Rais Samia alijibu maelezo hayo - siku hiyohiyo ambayo Ndugai alitoa kauli yake, pasipo kutaja jina na kusema kwamba serikali itaendelea kukopa kwa ajili ya kuleta maendeleo hata kama kuna watu wanatoa kauli za kukatisha tamaa. Rais alisema nchi imekuwa ikikopa tangu utawala wa Awamu ya Kwanza na kushangaa kwamba inakuwaje watu wanahoji wakati huu.

Siku moja baada ya kauli ya Samia, makundi mbalimbali ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yalianza kutoa kauli za kumpinga Ndugai na kutaka achukuliwe hatua kutokana na kauli yake hiyo dhidi ya Rais wake. Ilimchukua Ndugai siku tano kutoa maelezo ya kuomba msamaha kutokana na kauli yake ya awali.

Image: IKULU

Katika maelezo yake kwa waandishi wa habari katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma, Ndugai alisema kwamba video iliyosambazwa na vyombo vya habari kwenye mkutano ambapo alisikika akikosoa mikopo "haikuwa halisi" lakini akasema anaomba msamaha kwa Rais, Mwenyezi Mungu kutokana na kauli yake hiyo.

Pamoja na msamaha huo wa hadharani, Januari 4 mwaka huu, Samia alizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam na kutoa maelezo ya kuonyesha kutofurahishwa na maneno ya Ndugai - safari hii akimtaja kwa cheo. Lugha ya maneno na mwili ya Rais Samia ilionyesha kwamba msamaha ulioombwa na Ndugai haukuwa umepokewa.

Tangu Samia azungume juzi, ilikuwa wazi kwamba kitanzi cha mnyongaji- kisiasa, kilikuwa kinatembea juu ya kichwa cha Ndugai ambaye amekuwa mbunge tangu mwaka 2000 na amewahi kuwa Naibu Spika wa Bunge kati ya mwaka 2010 hadi mwaka 2015.

Katika nchi ambayo mfumo wake wa kidemokrasia ni ule wa chama hodhi (dominant party system) kama ilivyo Tanzania- si rahisi kwa kiongozi mwingine wa nchi - iwe serikalini au katika mojawapo ya mihimili ya dola, kushindana nguvu na Rais aliye madarakani na kushinda. Haijawahi kutokea na katika namna mfumo wa sasa CCM na dola ulivyofumwa, si rahisi kutokea kwa nchi hii.

Hali halisi ni kwamba wakati wa utawala wa hayati Rais John Magufuli, alijitengenezea maadui wengi ndani na nje ya Bunge, hakutengeneza marafiki wa kisiasa wa kumkinga kwenye nyakati ngumu na alichagua wakati mbaya wa kutoa matamshi aliyoyatoa Dodoma. Kama asingefanya makosa ya kujiegemeza na Ikulu ya Magufuli kupita kiasi na kama angekuwa na marafiki wa maana wa kumtetea bungeni na nje huenda angeweza kuvuka upepo huu.

Tofauti ya Ndugai na Maspika wa Bunge la Tanzania

Kisiasa nchini Tanzania - taasisi mbili za Bunge na Urais zimekuwa zikiishi kwa kuheshimiana lakini mara zote Rais akiwa na mamlaka makubwa zaidi. Hii ni kwa sababu, kuanzia katika zama za chama kushika hatamu, Rais wa nchi alikuwa pia ndiye Mwenyekiti wa CCM (chama tawala); chombo kilichokuwa cha juu kuliko vyote ndani ya nchi.

Ndugai ni Spika wa kipekee katika historia ya Bunge la Tanzania. Yeye ana nakisi kadhaa ambazo watangulizi wake hawakuwa nazo kiuongozi. Spika wa kwanza wa Bunge la Tanzania huru, Adam Sapi Mkwawa, aliyeongoza kwa takribani miongo mitatu - alikuwa na sifa kubwa mbili; kwanza alikuwa Chifu mwenye heshima kubwa kutoka katika kabila la Wahehe lakini pia akiwa na historia ya kuwa mmoja wa watu weusi wa kwanza kuingia bungeni katika historia ya Tanganyika (Tanzania). Yeye na Chifu Abdieli Shangali wa Uchagani ndiyo walikuwa weusi wa kwanza kuingia bungeni wakati huo likiitwa Baraza la Kutunga Sheria mnamo mwaka 1947.

Image: BUNGE/TANZANIA

Mkwawa alikuwa akiheshimika kwa sababu hakukuwa na mbunge mwingine aliyekuwa amewahi kuingia bungeni kabla yake. Hata Baba wa Taifa, Julius Nyerere, alianza kujihusisha na siasa wakati Mkwawa tayari mbunge na mwanasiasa anayejulikana. Hili lilijenga heshima baina ya wawili hao - ikisadifu pia kwamba Nyerere alitoka katika ukoo wa kichifu pia.

Spika wa Bunge wa pili, Chifu Erasto Mang'enya, naye alikuwa kiongozi wa kijadi wa kabila la Wabondei lakini aliyekuwa na sifa ya kushiriki katika harakati za kuwania Uhuru wa Tanganyika; akiwa mmoja wa Watanzania wa awali kabisa kuwa na elimu ya shahada ya kwanza (degree). Mwalimu Nyerere alimheshimu kwa elimu yake na maarifa aliyokuwa nayo.

Spika wa Bunge wa tatu, Pius Msekwa, hakuwa Chifu wala mbunge kama Mkwawa. Lakini wakati anaanza kuwa Spika kwenye miaka ya 1990, tayari alikuwa akionekana kama mtu anayelifahamu Bunge la Tanzania pengine kuliko yeyote mwingine. Alikuwa Katibu wa Bunge baada ya Uhuru na hivyo alikuwa kama mkunga wa taasisi hiyo kiutawala. Hakukuwa na mtu aliyekuwa na shaka juu ya umahiri wake kwenye Bunge.

Spika wa Bunge wa nne, Samwel Sitta, alikuwa na faida ya kuwa swahiba wa kisiasa wa Rais Jakaya Kikwete aliyeshiriki katika mapambano ya kumwingiza madarakani. Kwa sababu hiyo, Uspika wake ulikuwa na mamlaka kwa sababu alikuwa na nguvu kama swahiba wa Rais lakini pia mwanasiasa mkongwe aliyeingia bungeni miaka 30 kabla hajawa Spika.

Spika wa Bunge wa tano, Anne Makinda, hakuwa na ukaribu na Kikwete kama ule aliokuwa nao sita, lakini yeye alikuwa na uzoefu wa takribani miongo 40 ndani ya Bunge - akiwa ametumikia takribani mawaziri wakuu watatu - Edward Sokoine, Salim Ahmed Salim na Cleopa Msuya - kama Waziri wa Nchi (Bunge) na CCM ikimnadi kwamba ilitaka Spika wa Bunge mwenye jinsia ya kike. Hakukuwa na mwanasiasa mwanamke aliyekuwa na 'sifa' zilizotakiwa wakati ule kuwa Spika kumzidi Makinda.

Ndugai alipata Uspika kwa sababu ya siasa za uchaguzi za Bunge. Hakuwa na Uchifu wa Mkwawa, uzoefu wa Msekwa, bahati na umahiri wa Makinda wala ushawishi wa Sitta. Alikuwa amewahi kuwa Naibu Spika wa Bunge - sifa mojawapo ya watangulizi wake wawili waliokuja kuwa maspika baadaye; lakini Unaibu pekee si sifa ya moja kwa moja ya kumfanya mtu kuwa Spika. Hayati Sitta alikuwa Spika pasipo kuwahi kuwa Naibu.

Hili lilimaanisha kwamba Ndugai hakuwa na pa kushika kama ngome yake na baadaye alifanya uamuzi wa kuamua kuegemea kwenye mamlaka ya Rais Magufuli. Lakini, tofauti na Sitta ambaye alishiriki kwenye kumpambania Kikwete ashinde urais - Ndugai hakuwa sehemu ya kampeni ya Magufuli wala mmoja wa watu wake wa karibu. Kifo cha Magufuli Machi mwaka jana kilimaanisha kuanguka kwa nguzo kuu ya ukubwa wake bungeni.

Katika sintofahamu hii ya sasa na Rais Samia, Ndugai asingeweza kushinda wala kupambana kwa sababu hana kambi ya kumpambania. Kwa upande mwingine, Samia ana chama na serikali zilizo nyuma yake kwa sababu ya wadhifa wake kama Mwenyekiti wa chama na Rais. Kwa vyovyote vile, kulikuwa na mshindi mmoja tu kwenye hili naye ndiye aliyeamua namna ya kumaliza jambo hili - Rais.

Nini hasa kinaendelea?

Kuna wanaoamini kwamba kinachoendelea sasa kinaonyesha mgogoro ndani ya CCM lakini ukweli ni kwamba hii ni sawa na tufani kwenye kikombe (a storm in a tea cup). Kuna makundi maslahi ndani ya CCM ambayo yanaweza kuzusha mgogoro lakini si kati ya Mwenyekiti wa chama tawala na Spika wa Bunge ambaye nguvu yake iliyompa ukuu imeondoka tayari.

Kuna wanaozungumza kuhusu kile kinachoitwa "Sukuma Gang" kuwa nguvu iliyo nyuma ya upinzani dhidi ya Samia ndani ya CCM kwa sasa. Kundi hilo, nguvu yake kubwa ilikuwa Rais Magufuli mwenyewe na bila yeye kundi hilo halina kiongozi, itikadi wala ushawishi. Kama hatimaye Samia atapata upinzani ndani ya chama chake, hautatokana na "Sukuma Gang" bali na makundi mengine ya kudumu yaliyo ndani ya chama hicho.

Kinyume chake, sakata hili linatoa nafasi kubwa mbili kwa CCM na Samia - mosi linampa Rais nafasi ya kupata Spika anayemtaka na pengine Baraza la Mawaziri analolitaka mwenyewe. Hili litasimika nguvu ya Samia bungeni na kwenye Baraza la Mawaziri.

Pili, hatua ya viongozi wa mikoa na jumuiya za CCM kuanza kufanya mikutano na waandishi wa habari kuzungumzia masuala ya Ndugai na mengine inaonyesha kurejea kwa siasa zilizo zoeleka ndani ya CCM. Kwenye utawala wa Magufuli, ilionekana kama CCM iliyozoeleka ilianza kupotea na nguvu ya zamani ya viongozi wa chama wa mikoa, wilaya na jumuiya ilianza ilisinyaa.

Ni kama vile sakata hili limetoa nafasi kwa CCM kuanza kujichipua tena kama chama kinachofanya siasa kama ilivyokuwa wakati wa utawala wa Rais Jakaya Kikwete na watangulizi wake tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi. Kwa maneno mengine, sakati hili linamfanya Samia sasa aonekane kama mtu anayerejesha chama kwa "wenyewe".

Baada ya kumalizika kwa sakata hili la sasa-kutakuwa na mshindi mmoja tu; bungeni, kwenye baraza la mawaziri na ndani ya CCM - Samia Suluhu Hassan.