Wanafunzi 6 wakamatwa kwa kuchoma shule iliyo karibu na Ikulu

Muhtasari

•Imeripotiwa kwamba vitanda nane vilikuwa vimechomeka tayari kabla ya moto kuweza kudhibitiwa.

Moto mkubwa
Moto mkubwa
Image: WIKIPEDIA

Wanafunzi sita wa shule ya upili ya Milimani iliyo karibu na Ikulu ya Nairobi wametiwa mbaroni baada yao kujaribu kuteketeza bweni usiku wa Jumapili.

Polisi na usimamizi wa shule wamesema tukio la Jumapili lilikuwa jaribio la pili la kuteketeza bweni kutokea shuleni humo.

Imeripotiwa kwamba vitanda nane vilikuwa vimechomeka tayari kabla ya moto kuweza kudhibitiwa.

Wavulana hao walikuwa wamefanya jaribio kama hilo Ijumaa iliyopita lakini lilikatizwa na usimamizi wa shule.

Polisi waliitiwa ili kukamata vijana hao baada ya moto kuzimwa.

Hii ni shule ya pili kuathiriwa na tukio kama hilo katika kipindi cha wiki moja ambacho kimepita.

Shule nyingine ya kibinafsi katika eneo la Utawala iliathirika wiki iliyopita kabla ya wasichana nane waliohusishwa na tukio hilo kukamatwa.

Vijana waliokamatwa wanaendelea kuhojiwa kabla ya kufikishwa mahakamani.

Hii ni shule ya hivi majuzi kuripoti kisa cha uchomaji huku zaidi ya shule 100 zikiwa zimeathirika katika kipindi cha miezi minne ambacho kimepita.