Seneta Linturi aachiliwa kwa bondi ya Sh5M katika kesi ya uchochezi

Muhtasari

•Hakimu Mkuu wa Nakuru Edna Nyaloti ameamuru seneta huyo kutowasiliana na mashahidi kwa njia yoyote ile iwe ni moja kwa moja au kupitia wakala.

Seneta wa Meru Mithika Linturi ameachiliwa kwa bondi ya Sh5 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho na dhamana mbadala ya Sh2milioni pesa taslimu.
Seneta wa Meru Mithika Linturi ameachiliwa kwa bondi ya Sh5 milioni na mdhamini wa kiasi sawa na hicho na dhamana mbadala ya Sh2milioni pesa taslimu.
Image: Jeptum Chesiyna

Seneta wa Meru Mithika Linturi ameachiliwa kwa dhamana ya pesa taslimu shilingi milioni mbili au mdhamini wa kiasi cha shilingi milioni 5 kutokana na matamshi yake ya chuki aliyotoa mjini Eldoret.

Hakimu Mkuu wa Nakuru Edna Nyaloti ameamuru seneta huyo kutowasiliana na mashahidi kwa njia yoyote ile iwe ni moja kwa moja au kupitia wakala.

Nyaloti alisema hakuna ushahidi wa kutosha kuzuia uhuru wa mshtakiwa kabla ya kufunguliwa mashtaka.

Amesema serikali ina mitambo ya kuendelea na uchunguzi bila kumnyima mwandani huyo wa naibu rais uhuru wake.

Hali kadhalika amesema serikali inaweza kumfuatilia seneta Linturi na hata kuingilia mawasiliano yake.

Linturi alikamatwa siku ya Jumapili kufuatia matamshi ambayo alitoa alipokuwa anahutubia wafuasi wa naibu rais William Ruto mjini Eldoret.

Matamshi ya Linturi 'madoadoa' yalikosolewa na yanaendelea kukosolewa sana na Wakenya ikiwemo viongozi wa hadhi mbalimbali.

"Sisi tunataka kuwa kwa serikali inayokuja lakini nawaambia watu wa Uasin Gishu msicheze na Kenya na kile nawaomba ni kwamba madoadoa yale mliyonayo hapa muweze kuondoa. Hatuwezi kuwa tukisimama na William Ruto kule Mt Kenya na mko na wengine hapa hawasikii na hawawezi ungana naye...". Linturi alisikika akisema.

Mnamo Jumatatu naibu rais William Ruto aliomba radhi kufuatia matamshi hayo ya mwandani wake.

Kesi ya Linturi itatajwa tena mnamo Januari 26.