Mwanaharakati kortini kusitisha mashtaka ya matamshi ya chuki dhidi ya Onyonka

Muhtasari
  • Mwanaharakati kortini kusitisha mashtaka ya matamshi ya chuki dhidi ya Onyonka
Richard Onyonka
Richard Onyonka
Image: twitter/ Richard Onyonka

Mwanaharakati amehamia kortini akitaka kumzuia Mbunge wa Kitutu Chache Kusini Richard Onyonka kushtakiwa kwa matamshi ya chuki.

Fredrick Bikeri alidai kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji hana mamlaka ya kuelekeza Inspekta Jenerali wa Polisi kuchunguza matamshi ya chuki na makosa ya uchochezi.

Onyonka alikamatwa Jumanne baada ya DPP kuagiza IG Hilary Mutyambai achunguze matamshi aliyotoa.

Kupitia kwa wakili wake Danstan Omari, Bikeri anabisha kwamba maagizo ya Haji ni kinyume cha sheria na kwamba ni Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano pekee ndiyo inaweza kutoa agizo kama hilo.

Bikeri alisema hatua za DPP ni kosa la kisheria ambalo linadhoofisha utawala wa sheria.

Omari alidai kuwa kuna haja kubwa ya kuwa na akili timamu kukuzwa ndani ya mipaka, hasa kwenye uchunguzi na kuwafungulia mashitaka wenye chuki ili kuepusha matukio ambapo watu wataachiliwa huru kwa masuala ya kiufundi.