Polisi 4 wauawa katika shambulizi la Al-Shabaab Garissa

Muhtasari

•Washambuliaji hao wanaoaminika kuwa wanamgambo wa al-Shabaab na ambao walivuka kutoka mpaka wa karibu wa Kenya na Somalia walitoroka na bunduki za maafisa hao.

•Katika kaunti ya Wajir, magaidi walijaribu kuwateka nyara madiwani wawili wa zamani katika mtaa mmoja Jumapili jioni.

crime scene
crime scene
Image: MAKTABA

Maafisa wanne wa polisi waliuawa Jumatatu wakati gari walilokuwa wakisafiria liliposhambuliwa na watu waliojihami kwa bunduki katika eneo la Liboi, Kaunti ya Garissa

Maafisa hao walikuwa wakisafiri kwa gari aina ya probox walipojipata katika shambulizi hilo kati ya Liboi na eneo la Kulan.

Washambuliaji hao wanaoaminika kuwa wanamgambo wa al-Shabaab na ambao walivuka kutoka mpaka wa karibu wa Kenya na Somalia walitoroka na bunduki za maafisa hao.

Walioshuhudia walisema walisikia milio ya risasi kutoka eneo la Damajale na walipoenda kuangalia wakapata miili ya maafisa hao wanne hapo.

“Waliviziwa na kupigwa risasi kabla ya kuporwa silaha zao. Ilikuwa ni shambulizi la kuvizia,” alisema afisa anayefahamu kuhusu kisa hicho.

Maafisa hao waliporwa bunduki tatu aina ya AK47 na idadi isiyojulikana ya risasi.

Tukio hilo  ndilo la hivi punde kutokea katika eneo hilo.

Katika kaunti ya Wajir, magaidi walijaribu kuwateka nyara madiwani wawili wa zamani katika mtaa mmoja Jumapili jioni.

Wawili hao walifanikiwa kutoroka kutoka mikononi mwa watekaji nyara wakati waliwaacha kwenye gari na kwenda kusali.

Mkuu wa polisi katika eneo la Kaskazini Mashariki Rono Bunei alisema wameimarisha operesheni katika eneo hilo ili kudhibiti harakati za magenge hayo.

Kisa hicho kilijiri wiki moja baada ya polisi katika eneo hilo kupata vyakula na vifaa vingine ambavyo magaidi walikuwa wakitumia kabla ya kutoroka.

Hii ilitoa dalili ya shughuli na mipango yao katika eneo hilo.

Mauaji hayo yalijiri siku chache baada ya maafisa wanne kuuawa katika eneo la Milihoi, kaunti ya Lamu katika shambulizi kama hilo.

Serikali imeshutumu kuibuka kwa ukabila ambao unahusishwa na mielekeo ya kisiasa kuhusu uchaguzi, harakati inayokuja ya kusajili wapigakura na mizozo ya ardhi kama sababu kuu za mashambulizi ya hivi punde na watu kuhama Lamu.

Eneo hilo ni miongoni mwa zile zilizo chini ya amri ya kutotoka nje jioni hadi alfajiri.