Mlinzi afikishwa mahakamani kwa kupapasa matiti na makalio ya mhudumu wa hoteli

Muhtasari

•Karatasi ya mashtaka inasema mshtakiwa alimgusa JPN matako kwa mikono yake kinyume na kanuni za adhabu.

•Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo mbele ya Hakimu mkuu wa Kibera Derrick Kuto na kuachiliwa kwa bondi ya Sh300, 000

Dainon Lempirdaany katika mahakama ya Kibera
Dainon Lempirdaany katika mahakama ya Kibera
Image: CLAUSE MASIKA

Mlinzi mmoja anayedaiwa kumfanyia mwanamke mmoja kitendo kisicho cha heshima katika mkahawa aliokuwa akiulinda alifikishwa katika mahakama ya Kibera Jumatano na kufunguliwa mashtaka.

Kulingana na karatasi ya mashtaka,Dainon Lempirdaany, alitenda kosa hilo mnamo Januari 8 mtaani Lavington kando ya barabara ya Gitanga, kaunti ndogo ya Dagoretti, kaunti ya Nairobi.

Karatasi ya mashtaka inasema mshtakiwa alimgusa JPN matako kwa mikono yake kinyume na kanuni za adhabu.

Kulingana na wapelelezi, mlalamishi alikuwa kwenye hoteli moja na mlinzi huyo ambaye alidai apewe chai.

Polisi wanasema kuwa mwanamke huyo ambaye anafanya kazi ya uhudumu  katika hoteli hiyo alimwambia mshtakiwa kuwa hakukuwa na maziwa lakini akasisitiza apate chai na kumlazimisha amwandalie chai nyeusi.

“Sikujua kamwe kwamba walinzi wengine wawili hawakuwa wameripoti kazini. Mpangaji pia alikuwa hajaripoti kazini. Nilikuwa kazini na mshtakiwa,” mlalamishi alisema kwenye ripoti ya polisi.

Taarifa ya polisi inaongeza kuwa baada ya mshitakiwa kunywa chai, aliondoka na kurudi baadaye akidai chai zaidi ambayo aliahidi kulipia.

Mwanamke huyo aliwaambia polisi kwamba mshtakiwa alianza kummiminia maneno ya sifa akisema ni mkarimu, mrembo na ana umbo zuri huku akianza kumshikashika matako kwa mikono yake.

Alisema hiyo ilikuwa mara ya pili kwa mshtakiwa huyo kumfanyia vitendo hivyo. Mshitakiwa huyo alikamatwa kwa kosa hilo baada ya mwathiriwa kuwasilisha malalamiko yake kwa polisi na kupelekea kuwasilishwa kwake mahakamani.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo mbele ya Hakimu mkuu wa Kibera Derrick Kuto na kuachiliwa kwa bondi ya Sh300, 000 . Hakimu aliagiza kwamba kesi hiyo itajwe baada ya wiki mbili.

Kuto pia aliagiza mshtakiwa apewe taarifa za shahidi na ushahidi wa maandishi ambao upande wa mashtaka utategemea kesi nzima.