Jambazi auawa Githurai, 5 watoroka na majeraha ya risasi baada ya kuibia mwanafunzi mgeni

Muhtasari

• Ndegwa alikuwa mgeni katika maeneo ya Githurai na alikuwa ametoka katika hopitali ya chuo kikuu cha Kenyatta kupeleka barua ya kuomba kazi ya ndugu yake.

•Alipokuwa anatoka kwenye hoteli ile, majambazi wale walimshambulia kabla ya polisi waliokuwa wanashika doria kuskia nduru zake na kukimbia katika eneo la tukio.

Mtaa wa Githurai
Mtaa wa Githurai
Image: TWITTER// DCI

Jambazi mmoja aliuawa na wenzake watano wakafanikiwa kutoroka na majeraha ya risasi baada ya polisi kuwapata wakishambulia mwanafunzi wa chuo kikuu katika eneo la Githurai 44.

Genge la majambazi sita ambao walikuwa wamejihami kwa panga lilishambulia John Ndegwa 22, mwanafunzi katika chuo cha Sayansi na Teknolojia cha Kiambu na kumuibia Sh10, 000 pamoja na simu.

Kitengo cha upelelezi wa Jinai (DCI) kimeripoti kwamba Ndegwa alikuwa mgeni katika maeneo ya Githurai na alikuwa ametoka katika hopitali ya chuo kikuu cha Kenyatta kupeleka barua ya kuomba kazi ya ndugu yake.

Baada ya kufanikiwa kupeleka barua hiyo Ndegwa aliamua   kutembea  kando ya barabara kuu ya Thika akielekea Githurai huku akitafuta mahali pazuri pa kupata chakula cha mchana kwani ilikuwa mwendo wa saa nane alasiri.

Ndegwa alipofika katika eneo la Majengo alikutana na wezi ambao walimwagiza awanunulie sigara. Alitii agizo lao na kuwapa shilingi mia moja kabla yao kumruhusu aingie kwa hoteli apate chakula.

Alipokuwa anatoka kwenye hoteli ile, majambazi wale walimshambulia kabla ya polisi waliokuwa wanashika doria kuskia nduru zake na kukimbia katika eneo la tukio.

Wezi wale walipoona polisi walikimbia kuelekea pande tofauti kabla ya mmoja wao kutoa batola ya kujitengenezea na kupiga risasi kuelekeza upande waliokuwa polisi wale. Polisi nao hawakuchelewa kufyatua risasi zao na wakafanikiwa kumwangamiza  jamaa huyo anayeaminika kuwa kiongozi wao.

Polisi waliendelea kuwakimbiza wezi wale wengine ambao walifanikiwa kutoroka na majeraha mengi ya risasi. Vikosi mbalimbali vilitumwa katika eneo hilo kusaidia kuwasaka tano hao.

Simu ya mhasiriwa iliweza kupatikana mifukoni mwa mwizi aliyeuawa kisha mwili wake ukapelekwa katika City  Mortuary.