Hazina ya kitaifaya Bima ya Hospitali (National Hospital Insurance Fund ) sasa itajulikana kama Hazina ya kitaifa ya Bima ya Afya (National Health Insurance Fund).
Mwenyekiti wa bodi ya NHIF Lewis Nguyai alisema hazina hiyo itakuwa ikifanyia marekebisho kandarasi zake ili iitwe kandarasi ya mhudumu wa afya kati ya hazina ya kitaifa ya bima ya afya na watoa huduma za afya.
"Hatua hii inalenga kupanua mtandao wa wahudumu kwa sababu sio hospitali pekee zinazotoa huduma za afya, lakini kuna watoa huduma wengi wa afya na pia tutawajumuisha katika mikataba," Nguyai alisema.
"Hao wanaweza kuwa watu wa serikali na watu binafsi, zinaweza kuwa taasisi zinazotoa huduma za afya, linaweza kuwa duka la dawa, wanaweza pia kuwa watu wanaotumia teknolojia kutoa huduma za afya kama vile telemedicine," aliongeza.
Jina jipya pia linalenga kujumuisha mashirika ambayo yana vituo vya kusafisha damu kwenye figo, vituo vya huduma ya saratani na vituo vya utunzaji wa wagonjwa wa kisukari.
"Tulichofanya ni tumeangalia mtazamo kamili kuelekea utoaji wa huduma za afya. Sio hospitali pekee zinazowajibika kutoa huduma za afya. Kwa hivyo, ninaamini sasa tutaweza kufikia watu zaidi na kuweza kupanua hadi asilimia 100 ya Wakenya wanaofaidika na huduma za afya,” akasema.
Hazina hiyo kwa sasa inaendelea na msururu wa mageuzi ili kuhakikisha inakuwa endelevu kupitia utaratibu ambao una utambulisho na usajili wa walengwa.
Bima ya kitaifa ya afya imeonekana kama chombo cha kuafikia utoaji wa bima ya afya kwa wananchi Wote.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe aliunda jopo la wataalam wa mageuzi ya ufadhili wa afya ambalo lilibainisha masuala manne muhimu ya mageuzi, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hazina hiyo ili kuhakikisha kuwa ni linakidhi mahitaji ya walengwa.