Rais Kenyatta atia saini mswada wa vyama vya kisiasa kuwa sheria

Muhtasari
  • Rais Kenyatta atia saini mswada wa vyama vya kisiasa kuwa sheria
Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta leo katika Ikulu ya Nairobi ametia saini Mswada wa Marekebisho ya Vyama vya Kisiasa wa 2021 uliopitishwa hivi majuzi kuwa sheria.

Mswada huo wa bunge uliidhinishwa na Bunge la Kitaifa katika kipindi cha sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya kabla ya kuwasilishwa kwa Seneti ambapo ulipitishwa jana.

Sheria hiyo mpya inarekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2011 kwa kuanzisha dhana ya muungano wa vyama vya siasa, kuainisha kazi za vyama vya siasa pamoja na kubadilisha vigezo vya kupata Mfuko wa Vyama vya Siasa.

Sheria hiyo pia inampa Msajili wa Vyama vya Siasa mamlaka ya kuthibitisha orodha za wanachama wa vyama vya siasa na kanuni za uteuzi miongoni mwa vipengele vingine vya mageuzi vinavyolenga kuimarisha usimamizi wa vyama vya siasa na kuimarisha demokrasia.

Mswada huo uliwasilishwa kwa Rais ili kutiwa saini na Naibu Mkuu wa Wafanyikazi wa Ikulu Njee Muturi katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Dkt Joseph Kinyua, Spika wa Seneti Ken Lusaka, mwenzake wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi pamoja na Viongozi wa Wengi Bungeni Samuel Poghisio. (Seneti) na Amos Kimunya (Bunge la Kitaifa).

Pia walikuwepo Mwanasheria Mkuu Paul Kihara na Makarani Jeremiah Nyegenye (Seneti) na Michael Sialai (Bunge la Kitaifa).