Jinsi mwanajeshi wa KDF alivyoshirikiana na mpango wa kando kuua mkewe baada ya kufumaniwa

Muhtasari

•Inasemekana ugomvi ulizuka baada ya Phoebe kuwasili nyumbani Jumapili bila kusema na kumfumania Gitau na mwanamke mwingine.

•Gitau na mpango wake wa kando walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo huku uchunguzi wa maiti ukisubiriwa.

Crime scene
Crime scene

Mwanajeshi wa KDF na mpenzi wake walikamatwa Jumapili kuhusiana na mauaji ya mwanajeshi wa kike katika eneo la Utawala, Nairobi.

Mwanajeshi aliyeuawa alitambulishwa kama Phoebe Kaele na alikuwa anafanya kazi katika kituo cha Modica, Garissa ilhali mpenzi wake John Gitau alifanya kazi katika kituo cha Embakasi, Nairobi.

Inasemekana ugomvi ulizuka baada ya Phoebe kuwasili nyumbani Jumapili bila kusema na kumfumania Gitau na mwanamke mwingine.

Inaripotiwa kuwa mgeni huyo alikuwa amejificha wakati Phoebe aliingia ila viatu vyake vilikuwa mlangoni.

Phoebe alitaka kujua mwenye viatu hivyo na hapo vita vikazuka.Gitau anaripotiwa kuchukua kisu na kumdunga mpenzi huyo wake na kumuua papo hapo.

Kwa kushirikiana na mpango wake wa kando walijaribu kusafisha mahali ambapo damu ya marehemu ilikuwa imemwagika na kuficha mavazi yake ambayo yalikuwa yamelowa damu.

Gitau aliishi kwa nyumba ya kukodisha nje ya kambi ya jeshi. Baada ya kutekeleza mauaji hayo alimpigia mwanajeshi mwenzake na kumfahamisha kuhusu tukio hilo.

Baadae mwanajeshi huyo mwenzake aliwafahamisha polisi ambao walifika katika eneo la tukio na kupata mwili wa Phoebe ukiwa umelala juu ya kiti.

Polisi walifanikiwa kupata silaha ya mauaji na nguo ambazo zilikuwa zimelowa damu zimewekwa ndani ya ndoo na kufichwa bafuni. Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Gitau na mpango wake wa kando walikamatwa kuhusiana na mauaji hayo huku uchunguzi wa maiti ukisubiriwa.