Mike Sonko ajiuzulu kutoka chama cha Jubilee

Muhtasari

•Sonko  amesisitiza kuwa kubanduliwa kwake mamlakani mwaka wa 2020 kulikuwa kinyume na sheria na kwenye nia mbaya.

•Haya yanajirisiku chache tu baada ya mwanasiasa huyo na familia yake kupigwa marufuku kuingia Marekani.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: Facebook// Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Gideon Mbuvi almaarufu Mike Sonko amewasilisha barua ya kujiuzulu kutoka chama tawala cha Jubilee.

Katika barua hiyo iliyoandikwa Machi 10, Sonko alishukuru chama cha Jubilee kwa kumuunga mkono alipokuwa anahudumu kama gavana wa kaunti ya jiji kuu la Kenya.

Sonko pia  alisisitiza kuwa kubanduliwa kwake mamlakani mwaka wa 2020 kulikuwa kinyume na sheria na kwenye nia mbaya.

"Tafadhali kubali barua hii kama notisi yangu rasmi ya kujiuzulu kama mwanachama wa Jubilee kuanzia tarehe 10 Machi 2022. Hii ni katika kutekeleza haki zangu za kuwa mwanachama wa chama cha kisiasa ninachokichagua kama ilivyobainishwa chini ya Katiba ya Kenya. Ningependa kushukuru  uongozi wa chama kwa kuniunga mkono wakati wa utawala wangu kama gavana wa Nairobi kabla ya kuondolewa mamlakani na natumai watasaidia  kubadili hilo kwa ubora. Natakia chama na wanachama wake mema siku za usoni," Barua ya Sonko ilisoma.

Haya yanajiri siku chache tu baada ya mwanasiasa huyo na familia yake kupigwa marufuku kuingia Marekani.

Sonko ambaye anatazamia kujaribu kiti cha ugavana wa Nairobi kwa mara nyingine  alitaja hatua hiyo kama njama ya kujaribu kuangamiza azma yake ya kisiasa.