Moses Kuria abadili msimamo, aapa kupigia debe BBI

Muhtasari

•Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto amesema tatizo kubwa la BBI lilikuwa mchakato wake ila sio maudhui yake.

Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria
Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria
Image: MAKTABA

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, ameapa kuwa katika mstari wa mbele kupigia debe BBI ikiwa mahakama ya upeo itaidhinisha mchakato wake.

Mwandani huyo wa naibu rais William Ruto amesema tatizo kubwa la BBI lilikuwa mchakato wake ila sio maudhui yake.

"Tatizo la BBI halikuwa maudhui pekee; lilikuwa ni mchakato. Athari halisi ya uamuzi wa mahakama ya upeo leo ​​itakuwa suluhu kwa matatizo yote ya mchakato. Ikiwa mahakama ya upeo itaamuru kupendelea BBI, hiyo itasafisha mchakato huo," Kuria alisema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Kuria ambaye ni mmoja wa wanasiasa waliopinga vikali BBI mwaka jana amesema yupo tayari kusukuma utekelezaji wake mara moja mahakama ikiipitisha.

Mahakama ya juu zaidi inatarajiwa kutoa uamuzi wake kuhusu BBI hivi leo, takriban miezi saba baada ya mahakamu kuu kutupilia mbali mchakato huo.