Watahiniwa wa KCPE kujua Sekondari watakazojiunga nazo wiki ijayo- Magoha

Muhtasari

•Waziri wa Elimu George Magoha amesema wanafunzi wote takriban milioni 1.2 watajiunga na kidato cha kwanza chini ya sheria mpya.

•Kulingana na Magoha, hatua kali zitachukuliwa ili kuhakikisha shule zote za kitaifa nchini zina mtazamo wa kitaifa katika suala la uwakilishi.

Waziri wa Elimu George Magoha akihutubia wanahabari Kisumu mnamo Machi 21, 2022.
Waziri wa Elimu George Magoha akihutubia wanahabari Kisumu mnamo Machi 21, 2022.
Image: FAITH MATETE

Watahiniwa wa mtihani wa KCPE 2021 waliopokea matokeo yao wiki jana watajua shule za upili walizochaguliwa kujiunga nazo wiki ijayo.

Waziri wa Elimu George Magoha amesema wanafunzi wote takriban milioni 1.2 watajiunga na kidato cha kwanza chini ya sheria mpya.

Magoha alikuwa akizungumza katika shule ya upili ya Kenya High ambapo alizindua darasa la CBC.

Hapo awali, Magoha alitangaza kuwa uteuzi huo utafanywa kwa njia ya haki na bila upendeleo.

Kulingana na Magoha, hatua kali zitachukuliwa ili kuhakikisha shule zote za kitaifa nchini zina mtazamo wa kitaifa katika suala la uwakilishi.

Watahiniwa watano bora wa jinsia zote kutoka kila kaunti ndogo watawekwa katika shule za kitaifa kulingana na chaguo walizofanya wakati wa kujiandikisha kwa mtihani wa KCPE.

Jumla ya watahiniwa 1,214,031 walifanya mtihani wa KCPE wa 2021.

Jumla ya watahiniwa 11,857 walipata kati ya alama 400 na 500 katika mtihani huo. Waliopata kati ya alama 300 na 399 ni 315,275. Wengine 578,197 walipata kati ya alama 200 na 299.

Watahiniwa waliopata alama 380 na zaidi watatarajia kuwekwa katika shule za kitaifa na za ziada za kaunti.