Nelson Havi atishia kuishtaki Safaricom

Muhtasari

• Aliyekuwa Rais wa LSK Nelson Havi ametishia kuishtaki kampuni ya Safaricom endapo watakatisha huduma ya  laini yake kwa kukosa kujisajili upya.

• "Mna Kitambulisho changu ambacho nilitumia kusajili kadi yangu. Nitawachukulia hatua za kisheria, endapo laini yangu itakatwa," alisema.

Aliyekuwa Rais wa LSK Nelson Havi ametishia kuishtaki kampuni ya Safaricom endapo watakatisha huduma ya  laini yake kwa kukosa kujisajili upya.

Kupitia  ujumbe wake katika mtandao wa Twitter siku ya Ijumaa, Havi alikiri kuwa amepokea ujumbe  kutoka kwa Safaricom ikimuelekeza kusajili laini yake.

Hata hivyo, aliiambia kampuni hiyo kuwa tayari wana  taarifa muhimu zinazohitajika kwa usajili huo na kuongeza kuwa atachukua hatua za kisheria endapo watakatisha huduma hiyo.

"Mna Kitambulisho changu ambacho nilitumia kusajili kadi yangu. Nitawachukulia hatua za kisheria, endapo laini yangu itakatwa," alisema.

Aidha Havi alitoa wito kwa Wakenya kutoruhusu kushtakiwa kwa zoezi la usajili.

Alitaja zoezi hilo kuwa haramu na lisilo la lazima akisema hakuna mtu anayestahili kulipa chochote kwa huduma hiyo.

"Hakuna Mkenya anayefaa kulazimishwa kugharamikia hata shilingi moja zaidi na wahudumu wa rununu. Acha tuone iwapo Safaricom itakata huduma kwa zaidi ya wakenya milioni 10 iwapo tutaghairi amri hizi ambazo ni kinyume cha sheria," Havi alisema.

Matamshi yake yanafuatia agizo lililotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini Kenya iliyoagiza watoa huduma wote wa simu kusajili wateja wao upya kwa mujibu wa sheria ifikapo Aprili 15.

Kulingana na CA, kadi zote za simu  ambazo hazijasajiliwa nchini Kenya zitazimwa baada ya muda wa makataa kuisha.

Maagizo hayo mapya ya usajili yanalenga kuongeza mapambano dhidi ya uhalifu na kuboresha usahihi wa data.

Mamlaka ya mawasiliano [CA] iliamuru waendeshaji wote wa mtandao wa simu kuharakisha zoezi la kusafisha data, na kuongeza kuwa hakuna muda zaidi utakaoongezwa.

Hii ni mara ya tatu katika muongo mmoja mdhibiti anakuja na tarehe ya mwisho ya kuzima baada ya jaribio kama hilo mnamo 2012 na 2018.

Mamlaka ya Mawasiliano imewataka watumiaji wengi walio na kadi za simu  zilizotumika kwa zaidi ya miaka 10 kutembelea watoa huduma wao ili kuchambua  data zao.