Seneta Kihika apuuzilia mbali madai ya kuwa jasusi wa Jubilee katika UDA

Muhtasari

•Kihika alisema amewasamehe wale walioeneza ripoti hizo akisema kuwa ni mambo ya kawaida katika msimu wa kisiasa.

•Kihika hata hivyo ameshikilia kuwa yuko katika chama cha UDA na anaunga mkono azma ya naibu rais William Ruto kuwania urais.

Seneta wa Nakuru Susan Kihika
Image: Hisani

Seneta wa kaunti ya Nakuru, Susan Kihika amepuuzilia mbali madai kuwa yeye ni jasusi wa Jubilee katika chama cha UDA.

Katika  taarifa yake ya Ijumaa jioni, Seneta huyo wa muhula wa kwanza alikanusha madai hayo na kusema kuwa ya ni ya kipuuzi.

"Waah nimeshutumiwa kwa uwongo kwa mambo mengi katika taaluma yangu ya kisiasa lakini sijawahi kuwa jasusi wa Jubilee katika UDA, haithuru (haijalishi)," alisema.

Kihika alisema amewasamehe wale walioeneza ripoti hizo akisema kuwa ni mambo ya kawaida katika msimu wa kisiasa.

"Ni msimu wa kisiasa wa kiasi cha hali ya juu ambapo chochote kinafanyika. Lakini ni sawa. Nimewasemehe. Mungu mbele," alisema.

Hapo awali, Mbunge wa Naivasha, Jane Kihara alimshutumu Kihika kwa kukutana na viongozi wa Chama cha Jubilee usiku na kuwaambia mambo ya ndani ya UDA.

"Seneta Susan Kihika hajasema ukweli na anaungana na wapinzani wetu wa kisiasa katika Jubilee Party ili kuhakikisha kwamba ni wagombeaji anaopendelea pekee wanapita," Kihara alisema.

Alidai mgombea huyo wa Ugavana wa Nakuru anamuunga mkono mpinzani wake katika nafasi ya ubunge wa Naivasha, John Kihagi wa Jubilee.

Kihika hata hivyo ameshikilia kuwa yuko katika chama cha UDA na anaunga mkono azma ya naibu rais William Ruto kuwania urais.

"Kwa kuondoa mashaka, hapa ndio tuko! Na hatusongi! Puuza propaganda ghushi za wanablogu waliokata tamaa! Ruto rais wa 5," alisema.