Spika wa Nairobi Benson Mutura kufikishwa mahakamani

Muhtasari

• Siku ya Alhamisi alihojiwa kwa saa kadhaakatika makao makuu ya DCI kwa madai ya kumuibia muajiri wake kwa kuitisha marupurupu ya usafiri na ilhali hakusafiri. 

Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura akiongoza kikao cha mawasilisho mnamo Oktoba 26, 2021 katika vyumba vya bunge. Picha: FI
Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi Benson Mutura akiongoza kikao cha mawasilisho mnamo Oktoba 26, 2021 katika vyumba vya bunge. Picha: FI

Spika wa bunge la kaunti ya Nairobi Benson Mutura anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo Ijumaa kujibu madai ya wizi.

Mutura alikesha katika seli za polisi baada kuhojiwa kwa muda mrefu na maafisa wa DCI.  

Mutura ambaye anakabiliwa na tuhuma za wizi alilala katika kituo cha polisi cha Muthaiga akisubiri kufikishwa mahakamani.  

Siku ya Alhamisi alihojiwa kwa saa kadhaakatika makao makuu ya DCI kwa madai ya kumuibia muajiri wake kwa kuitisha marupurupu ya usafiri na ilhali hakusafiri.  

Pia anakabiliwa na kosa la kuchukuwa kitambulisho cha afisa mmoja wa polisi aliyekwenda kumkamata siku ya Jumatano katika jumba la City Hall. 

Mutura alikuwa ameandamana na wakili wake alipoelekea katika makao makuu ya DCI mwendo wa saa tano mchana na kuhojiwa kwa takriban saa tano. 

Siku ya Jumatano Mutura alidai kwamba masaibu yake yalianza pale aliposema kwamba Nairobi Metropolitan Services ni taasisi haramu. 

"Kama ilivyo kwa sasa, NMs ni shirika lisilo halali kwani kuongezwa muda wake kuhudumu hakukufuata sheria," alibainisha. 

Mutura, ambaye ni mbunge wa zamani wa Makadara alidai kwamba hatua ya kuongeza muda wa NMS ilifaa kuidhinishwa na bunge la kaunti.