"Ni uchungu kupoteza mtoto" Raila amfariji mbunge Sankok baada ya mwanawe kujipiga risasi

Muhtasari

•Mwanawe Sankok ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Kericho anaripotiwa kufariki baada ya kujipiga risasi akiwa nyumbani kwao eneo la Narok.

•Raila ametuma risala zake za rambirambi kwa mbunge huyo huku akimuomba Maulana aweze kujalia familia yake nguvu ya kuweza kukabiliana na majonzi.

Image: TWITTER// RAILA ODINGA

Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga amemfariji mbunge maalum David Sankok anapoomboleza mwanawe.

Raila ametuma risala zake za rambirambi kwa mbunge huyo huku akimuomba Maulana aweze kujalia familia yake nguvu ya kuweza kukabiliana na hali iliyowapata.

"Tafadhali pokea salamu za rambirambi kutoka kwa Mama Ida na mimi. Mungu aijalie ujasiri familia yako yote. Tunakuombea," Raila alimwambia Sankok.

Kinara huyo wa ODM alimhakikishia Sankok kuwa familia yake inasimama naye katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.

"Ni chungu sana kupoteza mtoto, na hata zaidi, ni vigumu kumzika; tunasimama nanyi katika kipindi hiki kigumu," Alisema Raila.

Sankok alimpoteza mwanawe wa kwanza siku ya Jumatatu.

Mwanawe Sankok ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika shule ya upili ya Kericho anaripotiwa kufariki baada ya kujipiga risasi akiwa nyumbani kwao eneo la Narok.

Inaripotiwa kuwa mbunge huyo hakuwa nyumbani wakati mwanawe alichukua bunduki yake na kujiangamiza nayo. Bado haijabainika kilichopelekea tukio hilo na polisi wanajaribu kuchunguza ikiwa ni ajali ama marehemu alikusudia kujitoa uhai.

Polisi pia wanajaribu kubaini jinsi kijana huyo wa maika 15 aliweza kufikia bunduki ambayo inapaswa kufungiwa ipasavyo. Kijana alichukua bunduki katika sefu ya bafu.

Raila amemwambia Sankok anafahamu uchungu wa kupoteza mtoto kwa kuwa pia yeye alifiwa na mwanawe wa kwanza Fidel Castro Odinga mwaka wa 2015.

Kiongozi wa KANU Gideon Moi pia amemfariji mbunge huyo  na kumtakia nguvu za kukabiliana na majonzi.

"Natuma salamu zangu za rambirambi kwa Mheshimiwa Sankok na familia yake kufuatia kifo cha mwanawe. Upo katika mawazo na maombi yetu Mheshimiwa katika kipindi hiki kigumu. Jipe moyo na upate faraja kwa Mungu Mwenyezi," Moi aliandika kwenye Twitter.