JSC yaidhinisha kutimuliwa kwa Jaji Said Chitembwe

Muhtasari

Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) imeidhinisha kuondolewa afisini kwa Jaji Said Chitembwe. 

Jaji Said Juma Chitembwe wakati wa mahojiano kwa nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Juu Mei 3. Picha: CHARLENE MALWA
Jaji Said Juma Chitembwe wakati wa mahojiano kwa nafasi ya Jaji wa Mahakama ya Juu Mei 3. Picha: CHARLENE MALWA

Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) imeidhinisha kuondolewa afisini kwa Jaji Said Chitembwe. 

Kupitia kwa Jaji Mkuu Martha Koome, Tume hiyo imemwandikia Rais Uhuru Kenyatta kwa hatua zaidi.

JSC ilisema kwenye taarifa Jumatano kwamba imeridhishwa na matokeo ya uchunguzi uliofanyiwa jaji huyo kufuatia maombi yaliyowasilishwa dhidi yake. 

Tume hiyo ilisema kuwa imetuma mapendekezo yake kwa Rais Uhuru Kenyatta ili achukuliwe hatua inavyotakiwa kisheria. Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko ndiye mlalamishi mkuu aliyemshutumu hakimu huyo kwa ufisadi.

Jaji mkuu Martha Koome aliwahakikishia Wakenya kujitolea kwa tume ya JSC kuhakikisha kuna uadilifu na uwajibikaji katika Idara ya Mahakama. 

“JSC ilizingatia ripoti ya jopo hilo kuhusu ombi la tume kwa hoja yake yenyewe na imeridhika kwamba ombi hilo limebaini sababu za kuondolewa kwa Chitembewe,” ilisema taarifa hiyo. 

Mnamo Novemba 2021, Jaji Mkuu Martha Koome alisema JSC itakutana ili kujadili ombi la kutaka kuondolewa afisini kwa Chitembwe kufuatia ufichuzi kuhusu utovu wa nidhamu na njama za kuvuruga kesi. 

Madai yalioibuliwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko yanaonyesha Jaji Chitembwe kama mhusika katika njama ya kuhujumu haki katika mzozo wa ardhi. 

"Tume ya Huduma ya Mahakama itakutana kujadili suala hilo kulingana na katiba yake na taratibu zilizowekwa kisheria," Koome alisema katika taarifa yake kuhusu suala la Chitembwe. 

Chitembwe alikana kuhusika na ufisadi, akisisitiza kuwa video hizo zilibadilishwa ili kutoa simulizi za uongo. Kundi moja la mawakili kupitia tawi la Nairobi LSK pia walikuwa wametaka jaji huyo aondolewe. 

Kabla ya hapo, watu wengine wawili walikuwa wamewasilisha maombi ya kutaka aondolewe afisini. Mmoja wa walalamishi katika kesi ya kutaka Jaji Said Chitembwe aondolewe madarakani kutokana na tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi alidai kuwa hakimu huyo alijaribu kumpa rushwa ili aondoe kesi.