Polisi wasaka jamaa aliyemjeruhi mkewe kwa nyundo na kisu - Kwale

Muhtasari

• Namubuya, 29, anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Lunga Lunga akiwa katika hali shwari. 

 

Crime scene
Crime scene

Maafisa wa upelelezi katika kaunti ya Kwale wanamsaka mwanamume anayedaiwa kumjeruhi mkewe ambaye waliachana naye kwa nyundo na kisu usiku wa kuamkia leo (Alhamisi). 

James Kimeu anasemekana kumdunga kisu Caren Namubuya kifuani na kumpiga kichwani mara kadhaa kwa nyundo kabla ya kukimbia, na kumwacha akiwa amepoteza fahamu kwenye dimbwi la damu. 

Mkurugenzi wa DCI George Kinoti alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa wawili hao walitengana kabla ya Kimeu, 35, kumwalika Namubuya nyumbani kwake kwa nia ya kutafuta maridhiano. 

“Hata hivyo, Kimeu alifunga mlango kwa kufuli na kumgeukia mwanamke huyo kwa kisu cha jikoni na nyundo,” Kinoti alisema. 

Kinoti alisema majirani waliosikia zogo hilo waliingia kwa nguvu ndani ya nyumba hiyo na kumpata mwathiriwa akiwa amelala sakafuni kwenye dimbwi la damu. 

Namubuya, 29, anaendelea kupata nafuu katika hospitali ya Kaunti Ndogo ya Lunga Lunga akiwa katika hali shwari. 

“Mwanaume huyo ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi ya Menzamwenye, hata hivyo alifanikiwa kutoroka na tangu sasa wapelelezi wameanza msako,” alisema.