DCI yapata naibu mkurugenzi mpya Hamis Masa

Muhtasari

• Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya Hamis Masa alipandishwa cheo kuchukua wadhifa wa naibu DCI katika mabadiliko yaliyotangazwa Alhamisi. 

• Hatua hii inafuatia kustaafu kwa Joseph Ashmalla kutoka kwa huduma baada ya kufikia umri wa kustaafu. 

Naibu mkurugenzi mpya wa Idara ya Upelelezi wa Jinai nchini (DCI) ametajwa katika mabadiliko yaliyotangazwa na mkurugenzi George Kinoti. 

Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya Hamis Masa alipandishwa cheo kuchukua wadhifa wa naibu DCI katika mabadiliko yaliyotangazwa Alhamisi. 

Hatua hii inafuatia kustaafu kwa Joseph Ashmalla kutoka kwa huduma baada ya kufikia umri wa kustaafu. 

Katika mabadiliko hayo, mkuu wa DCI katika Kitengo cha Polisi wa Viwanja vya Ndege (KAPU) Bernard Nyakwaka alihamishwa na sasa mkuu wa DCI katika kanda ya Kati Jinai (RCIO) akibadilishana na Geoffrey Kathurima. 

Mkurugenzi mpya wa wafanyikazi katika makao makuu ya DCI atakuwa Gideon Kibunja. Kibunja alichukua nafasi kutoka kwa Dkt. Wanderi Mwangi ambaye alihamishwa hadi Shirika la Reli na kuteuliwa afisa mkuu wa upelelezi wa Jinai (CCIO). 

Mkurugenzi mpya wa mafunzo atakuwa CCIO wa Railway anayeondoka John Kamau huku Samuel Kobina akihamishwa kutoka chuo cha DCI, na kuteuliwa mkuu wa DCI kaunti ndogo ya Langata. Kinoti alitaja mabadiliko hayo kuwa ya kawaida yanayolenga kuimarisha utendakazi katika idara hiyo. 

Masa ni mkurugenzi wa muda mrefu wa ANU na uteuzi wake unaonekana kama zawadi kwa kazi yake.