logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mauaji shuleni! Kijana amdunga kisu aliyekuwa mpenziwe baada ya kugundua amenyakuliwa na mwingine

Kiptoo alimdunga kisu Chelangat baada ya mahusiano yao kugonga ukuta.

image
na Radio Jambo

Yanayojiri06 May 2022 - 02:19

Muhtasari


•Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Kiptoo aliumwa sana baada ya kugundua kuwa marehemu alikuwa amenyakuliwa na jamaa mwingine baada yao kutengana

Polisi katika kaunti ya Kericho wanamzuilia kijana mmoja mwenye umri wa miaka 19 ambaye alimuua mwanadada aliyekuwa mpenziwe.

Tony Kiptoo anaripotiwa kumuua Irene Chelangat ,22, kwa kumdunga kisu kwenye upande wa kushoto wa kifua chake ya mahusiano yao kugonga ukuta.

Wawili hao walikuwa wanafunzi katika shule ya upili ya Kaben na walikuwa kwenye mahusiano kwa muda kabla ya kutengana na Chelangat kusonga mbele na maisha yake.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa Kiptoo alitenda unyama huo Jumatano asubuhi kabla ya masomo ya asubuhi kung'oa nanga.

Wanafunzi wenza walioshuhudia tukio hilo walimshambulia mshukiwa mara moja huku wengine wakipiga nduru na kuita mwalimu Kenneth Korir ambaye alikuwa katika zamu.

Bw Korir alikimbia katika eneo la tukio na kupata mshukiwa akipigwa na baadhi ya wanafunzi huku wengine wakijaribu kuokoa maisha ya mhasiriwa ambaye alikuwa anavunja damu sana.

Mhasiriwa alikimbizwa hospitalini ila kwa bahati mbaya alipofikishwa pale ikathibitishwa kuwa tayari amekata roho.

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Kiptoo aliumwa sana baada ya kugundua kuwa marehemu alikuwa amenyakuliwa na jamaa mwingine baada yao kutengana. Mshukiwa hakufurahia kuona Chelangat alikuwa na mpenzi mwingine ambaye tayari alikuwa amemnunulia simu.

Kutokana na hasira ya kuachwa, Kiptoo tayari alikuwa amempatia marehemu ilani ya kifo kwa kuandika R.I.P kwenye picha yake ambayo ilipatikana ndani ya chumba chake baadae.

Kiptoo anaripotiwa kutumia kisu cha mamake kutenda unyama huo. Kwa sasa wapelelezi wanafuatilia kibali cha kumzuilia mshukiwa ili waweze kutayarisha kesi nzito dhidi yake.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved