Kiongozi wa kijiji ampiga mkewe hadi kifo kwa kutoka kimapenzi na jamaa mwingine

Muhtasari

•Denis Okeyo anaripotiwa kumpiga mkewe bila huruma baada ya kushuku alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine.

•OCPD alisema mshukiwa alijisalimisha kwa chifu msaidizi ambaye alimpeleka katika kituo cha polisi cha Chemelil.

Wanakijiji waliopigwa na mshtuko katika nyumba ya marehemu katika kijiji cha Koguta huko Muhoroni mnamo Mei 7, 2022.
Wanakijiji waliopigwa na mshtuko katika nyumba ya marehemu katika kijiji cha Koguta huko Muhoroni mnamo Mei 7, 2022.
Image: FAITH MATETE

Biwi la simanzi limetanda katika kijiji cha Koguta, eneo la Muhoroni baada ya msimamizi wa kijiji mwenye umri wa miaka 36 kudaiwa kumpiga mkewe hadi kifo kufuatia madai ya kukosa uaminifu katika ndoa.

Denis Okeyo anaripotiwa kumpiga mkewe bila huruma Ijumaa usiku baada ya kushuku kuwa alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine.

Marehemu alikuwa na umri wa miaka 25.

OCPD wa Muhoroni David Muniu alithibitisha kisa hicho na kusema alipokea ripoti za tukio hilo la kinyama kutoka kwa chifu msaidizi wa Komuswa, Jack Mboha.

“Mwanamume huyo alishuku kuwa mkewe alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine na kutokana na hilo akampiga kikatili,” Muniu alisema.

Muniu alisema baada ya mshukiwa kugundua kuwa amemjeruhi mkewe na maisha yake yalikuwa hatarini, alimkimbiza katika hospitali ya misheni ya Kikatoliki iliyo Awasi.

Hospitali hiyo ilipendekeza mhasiriwa apelekwe katika Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga iliyoko Kisumu lakini akafariki alipofika.

OCPD alisema mshukiwa alijisalimisha kwa chifu msaidizi ambaye alimpeleka katika kituo cha polisi cha Chemelil.

"Kwa hivyo, kwa sasa yuko kizuizini huku uchunguzi ukiendelea," OCPD alisema.

Wanakijiji waliozungumza na vyombo vya habari siku ya Jumamosi walikuwa bado na mshtuko kufuatia tukio hilo.

Walisema hakuna mtu anayepaswa kujichukulia sheria mkononi.

"Hata kama ni suala la kutoka nje ya ndoa, alipaswa kumrudisha kwa wazazi wake badala ya kumuua," Rosila Akoth, rafiki wa karibu wa marehemu alisema.

"Ni siku ya huzuni kwetu kwa sababu tulikuwa na marehemu Ijumaa mchana wakati wa mkutano wetu wa kikundi na hatukujua hili lingempata," Margaret Juma aliongeza.

David Okello, mchungaji wa eneo hilo, aliwashauri wanandoa kutafuta viongozi wa kidini ili kusaidia kutatua tofauti zao za ndoa.

Alilaani tukio hilo na kusema ni makosa sana kwa mshitakiwa kujichukulia hatua mkononi.

Mwili wa marehemu umelazwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga.