Jamaa aliyedai Sonko alikosea kaburi la mamake aghadhabisha wazee wa Lamu

Muhtasari

•Alawy Badawy ambaye ni kiongozi wa jamii  amesema kauli ya Abubakar Aboud imewakasirisha wazee wa eneo hilo.

•Wazee wa Lamu pia walimuomba Sonko kufanya ziara katika visiwa hivyo ili waweze kumpa baraka zao.

Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko akimimina maji kwenye kaburi la mamake Saumu Mbuvi katika makaburi ya Kikowani siku ya Ijumaa.
Aliyekuwa Gavana wa Nairobi Mike Sonko akimimina maji kwenye kaburi la mamake Saumu Mbuvi katika makaburi ya Kikowani siku ya Ijumaa.
Image: JOHN CHESOLI

Wazee wa Lamu wamemuita jamaa aliyedai kuwa mgombea ugavana wa Mombasa Mike Sonko alitembelea kaburi lisilofaa akikusudia kusali katika eneo alilozikwa marehemu mama yake.

Alawy Badawy, ambaye ni mzaliwa wa Lamu na kiongozi wa jamii, alisema kauli ya Abubakar Aboud imewakasirisha wazee wa eneo hilo.

Alawy alisema mamake Aboud angali hai na anaishi Lamu.

“Hatua zitachukuliwa dhidi yake. Wameita familia yake na ameonywa,” alisema Badway katika mahojiano ya simu na Star.

Alisema wazee wa Lamu wanamtaka Aboud atoe maelezo ya kurekebisha na aeleze ni kwa nini alitoa kauli hiyo.

“Mamake anaishi Lamu. Tunaweza kuwapeleka wanahabari kwake sasa hivi,” alisema Badawy.

Wazee wa Lamu pia walimuomba Sonko kufanya ziara katika visiwa hivyo ili waweze kumpa baraka zao.

Aboud, anayetoka Kaunti ya Lamu, Jumamosi alimshutumu Sonko kwa kutumia kaburi la mamake (Aboud) kwa harakati za kisiasa.

“Hili ni kaburi la mama yangu, Mariam Ali. Alizikwa hapa miaka saba iliyopita,” alisema Aboud.

“Acha Sonko atafute kaburi la mamake. Sio huyu,” alisema Aboud aliyekuwa akitokwa na machozi.

Aboud alipotafutwa alikana kuwa yeye ndiye aliyetoa taarifa hiyo

"Lazima una nambari isiyo sahihi," alisema, kabla ya kuzima simu yake,"

Siku ya Ijumaa, Sonko alitembelea kaburi la mamake Saumu Mukami Mbuvi katika Makaburi ya Kikowani Muslim Cemetery akiwa na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na mgombea mwenza wake Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo.

Sonko alisema mamake alizikwa hapo mwaka wa 1997.

Ziara hiyo ilikusudiwa kuwa ya kisiasa kuthibitisha kuwa Sonko ni mkazi wa Mombasa na si mtu wa nje kama walivyodai wapinzani wake.

Mnamo Mei 2, Gavana wa Mombasa Hassan Joho, ambaye amekuwa akimpigia debe Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir alisema Mombasa haiwezi kuongozwa na watu wa nje.

Wafuasi wa Sonko, akiwemo aliyekuwa Seneta Mteule Emma Mbura, hata hivyo, walisema Sonko ambaye alizaliwa katika mtaa wa Majengo anakuwa mzaliwa wa Mombasa kwa vile mamake Saumu alikuwa wa jamii ya Digo.