Makiwa! Mbunge Rigathi Gachagua ampoteza kaka yake mkubwa

Muhtasari

•Rigathi amemwomboleza  marehemu kama kiongozi wa familia yao na kumshukuru Mola kwa miaka ambayo ameweza kuwa pamoja nao. 

•Reraini aliwahi kujaribu siasa na aliwania ubunge wa Mathira kwa tikiti ya Ford Asili katika uchaguzi wa 2013 ila akapoteza.

Marehemu James Reriani Gachagua
Marehemu James Reriani Gachagua
Image: HISANI

Familia ya mbunge wa Mathira Rigathi Gachugua inaomboleza baada ya kaka yake mkubwa James Reriani Gachagua kuaga dunia.

Akitangaza habari hizo za kuhuzunisha siku ya Jumapili, Rigathi alisema kakake alifariki baada ya kupambana na ugonjwa kwa muda mrefu.

Rigathi amemwomboleza  marehemu kama kiongozi wa familia yao na kumshukuru Mola kwa miaka ambayo ameweza kuwa pamoja nao. 

"Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya kaka yetu mkubwa na mkuu wa familia yote ya Gachagua, James Reriani Gachagua ambaye amekwenda kuwa na Bwana baada ya kuugua kwa muda mrefu kwa ujasiri," Rigathi alitangaza kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Rigathi hata hivyo hakufichua ugonjwa ambao kaka yake alikuwa anaugua. Reriani ameaga akiwa na umri wa miaka 78.

"Tunamshukuru Mungu kwa miaka 78 ambayo marehemu aliishi. Tunaombea familia yake huku tukianza mipango ya kumzika. Roho yake ipumzike kwa amani," Alisema Rigathi.

Haya yanajiri takriban miaka mitano baada ya kaka mwingine wa Rigathi, Nderitu Gachagua kuaga dunia kutokana na ugonjwa wa Saratani.

Nderitu alikuwa mwanasiasa maarufu na alikuwa gavana wa kwanza wa Nyeri. Alifariki bado akiwa mamlakani mnamo Februari 24, 2017.

Reraini pia aliwahi kujaribu siasa na aliwania ubunge wa Mathira kwa tikiti ya Ford Asili katika uchaguzi wa 2013 ila akapoteza.