Tulilia sana mshtakiwa alipoachiliwa huru- Mama ya ndugu waliouawa Kitengela azungumza

Muhtasari

•Wanjiru amesema kuwa ana wasiwasi mwingi kuhusu hatima ya kesi hiyo huku akidai kuwa huenda ikasahaulika.

•Bi Wanjiru amesema alishangazwa sana na hatua hiyo ya mahakama kwani hakutarajia mshukiwa mkuu wa mauji ya wanawe angewahi kuwa huru tena.

Bi Lucy Wanjiru aliyepoteza wanawe wawili Kitengela
Bi Lucy Wanjiru aliyepoteza wanawe wawili Kitengela
Image: RADIO JAMBO

Bi Lucy Wanjiru, ambaye ni mama ya ndugu wawili kati ya vijana wanne waliouawa Kitengela mwaka jana ameeleza kutoridhishwa kwake na jinsi kesi ya mauaji ya wanawe inavyoendelezwa.

Wanjiru amesema kuwa ana wasiwasi mwingi kuhusu hatima ya kesi hiyo huku akidai kuwa huenda ikasahaulika.

"Ninaogopa. Naona kama kuna mambo yanafichwa. Ni kama itasahaulika," Wanjiru alisema akiwa kwenye mahojiano na Lynn Ngugi.

Wanawe Wanjiru, Fredrick Muriithi na  Victor Mwangi walifariki mnamo Agosti 8, 2021 baada ya kushambuliwa na umati wa watu uliowashtumu kwa wizi wa mifugo. Waliuawa pamoja na marafiki wao wawili, Mike George na Nicholas Musa.

Mnamo Agosti 17 mwaka jana, polisi walimtia mbaroni jamaa aliyedaiwa kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji hayo. Benson Melonyie ole Mungai hata hivyo aliachiliwa kwa dhamana ya Ksh2M mwezi Machi mwaka huu.

Bi Wanjiru amesema alishangazwa sana na hatua hiyo ya mahakama kwani hakutarajia mshukiwa mkuu wa mauji ya wanawe angewahi kuwa huru tena.

"Mara ya mwisho nilipoenda mahakamani na baadhi ya marafiki wangu hatukuwa tunatarajia mshtakiwa angewachiliwa huru. Tulipata shida sana wakati huo kwa sababu hatukuwa tunatarajia huyo mtu apewe dhamana ya milioni 2. Tulilia sana pale nje. Tulihoji jinsi watu wale walienda na mtu wao na sisi tukaenda bila watoto wetu," Wanjiru alisema.

Mfanyibiashara huyo amedai kuwa jamaa wa mshukiwa waliwakejeli baada mahakama kumuachilia huru.

Ameeleza kusikitika kwake huku akisema bado hajaweza kupata haki ya wanawe. Ameeleza kusikitika kwake na kuweka wazi kuwa bado hajaweza kupata haki ya wanawe.

Wanjiru pia alifichua amekuwa akienda kwa mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia ili kupata usaidizi wa kukabiliana na majonzi ya kupoteza wanawe.