Mgomo wa wahudumu wa matatu wasababisha msongamano mkubwa Waiyaki Way

Muhtasari

•Wafanyakazi wa matatu walikuwa wakipinga kuondolewa kwa kituo cha mabasi kilichokuwa karibu na mzunguko wa Westlands ambao ulifungwa hivi majuzi.

•Polisi waliokuwa kwenye barabara hiyo waliwaelekeza madereva kutumia njia mbadala kufika walipokuwa wanaenda.

Msongamano mkubwa wa magari washuhudiwa Waiyaki Way mnamo Mei 19, 2022
Msongamano mkubwa wa magari washuhudiwa Waiyaki Way mnamo Mei 19, 2022
Image: PURITY WANGUI

Msongamano mkubwa wa magari ulishuhudiwa kwenye barabara ya Waiyaki Way jijini Nairobi Alhamisi asubuhi baada ya sehemu ya wahudumu wa matatu kugoma na kufunga barabara.

Polisi na maafisa wa GSU walilazimika kutumia vitoa machozi kutawanya umati wa watu waliokuwa wamekusanyika katika mzunguko wa Westlands.

Wafanyakazi wa matatu walikuwa wakipinga kuondolewa kwa kituo cha mabasi kilichokuwa karibu na mzunguko wa Westlands ambao ulifungwa hivi majuzi.

Wahudumu wa magari walifanya maandamano, wakizuia pande zote mbili za barabara, na kutatiza mwendo wa magari.

Baadhi ya watu wanaotumia barabara ya Waiyaki ambao walipatikana na msongamano huo walilazimika kutembea umbali mrefu  kufuatia usumbufu huo.

Polisi waliokuwa kwenye barabara hiyo waliwaelekeza madereva kutumia njia mbadala kufika walipokuwa wanaenda.

Waendesha magari waliopatikana na msongamano huo walionekana kughadhabishwa na tukio hilo ambalo lilichelewesha safari zao.