Tanzia: Uhuru amuomboleza mjukuu wa aliyekuwa shujaa wa ukombozi Dedan Kimathi

Muhtasari

• Rais Kenyatta alimtaja marehemu Teddy Mukaria kuwa mtu wa mwelekeo, manufaa na matumaini makubwa.

Rais Uhuru Kenyatta
Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ametuma ujumbe wa rambirambi kwa Mama Mukami Kimathi na familia yote ya shujaa wa ukombozi Dedan Kimathi kufuatia kifo cha mjuu wao Teddy Mukaria Githinji.

Katika ujumbe wake wa faraja na himizo siku ya Alhamisi, Rais Kenyatta alimtaja marehemu Teddy Mukaria kuwa mtu wa mwelekeo, manufaa na matumaini makubwa.

“Familia yangu na mimi mwenyewe tunahuzunishwa na msiba huo mkubwa. Akiwa na umri wa miaka 25 pekee, Teddy alikuwa mtu barubaru, mwenye mwelekeo, manufaa na matumaini makubwa. Aidha alikuwa kijana mwenye talanta aliyependa uhifadhi wa mazingira.

“Kifo chake ni pigo kubwa kwa familia ya Dedan Kimathi na namuomba Mwenyezi Mungu kuipa faraja wakati huu mgumu," kasema Rais.

Kiongozi wa Taifa alisema marehemu Teddy atakumbukwa kwa upendo kwa kuwa kielelezo bora zaidi kwa vijana.