Mwanadada akamatwa kuhusiana na Kokeini ya Ksh 100M iliyopatikana Mombasa

Muhtasari

•Kitengo cha DCI kimesema bado haijabainika ikiwa Cocaine hiyo ilikusudiwa kuuzwa hapa nchini ama kusafirishwa nje ya nchi.

Image: TWITTER// DCI

Polisi katika kaunti ya Mombasa wanamzuilia mwanamke mmoja anayehusishwa na biashara ya ulanguzi wa mihadarati aina ya Cocaine.

Nuru Murshin Mahfud ,29, alikamatwa Ijumaa kuhusiana na shehena ya Cocaine yenye dhamani ya Ksh100M ambayo ilipatikana ndani ya nyumba moja katika mtaa wa Utange, Mombasa.

Vikosi kutoka Kitengo cha  Uhalifu uliopangwa wa Kimataifa na kile cha Kupambana na Madawa ya Kulevya ambavyo vilitekeza operesheni hiyo vilipata dawa hizo zikiwa zimepangwa kwenye mifuko 35 ambayo ilikuwa imefichwa ndani ya  masanduku.

Kitengo cha DCI kimesema bado haijabainika ikiwa Cocaine hiyo ilikusudiwa kuuzwa hapa nchini ama kusafirishwa nje ya nchi.

Wataalamu katika maabara ya Kiforensiki ya DCI watazichunguza dawa hizo ambazo zinaripotiwa kuwa nyingi zaidi kuwahi  kupatikana siku za hivi majuzi.

Wapelelezi wanaendeleza uchunguzi  katika juhudi za kukamata washukiwa zaidi huku Mahfud akiwa amewekwa kizuizini akisubiri kushtakiwa.

Hii inamaanisha kuwa walangulizi wa dawa hizo zilizopigwa marufuku wanarejea baada ya muda mrefu.

Mnamo 2019, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Kenya Simon Mordue alisema bandari ya Kenya ya Mombasa ilichangia asilimia 30 ya heroini haramu iliyoingizwa katika soko la Umoja wa Ulaya. Alisema wameshirikisha mamlaka za Kenya kushughulikia suala hilo.

Mordue alisema wanafanya kazi kwa karibu na mashirika mbalimbali ili kubadili hali hii na kupata taarifa za kijasusi na polisi kuwakamata wafanyabiashara hao.

Taarifa hizo hazikuwa ngeni kwa baadhi ya viongozi wa serikali wanaofahamu mwenendo wa biashara hiyo.

Sehemu kubwa ya heroini nchini inatoka Afghanistan kupitia Bahari ya Hindi huku kokeini ikitokea Amerika Kusini.

Mashirika ya usalama ya Kenya yalinasa kokeini ya pili kwa ukubwa yenye uzito wa kilo 100 na yenye thamani ya Sh598 milioni mwaka wa 2016 mjini Mombasa ambayo ilikuwa imedaiwa  kuwa sukari. Kesi hiyo hata hivyo ilitupiliwa mbali kortini.