"Sitoi ata bob!" Sonko amwambia mwanadada anayemdai Sh448,450 kila mwezi za malezi ya mtoto

Muhtasari

•Sonko ameagiza mwanadada huyo amkabidhi mtoto huyo anayedai kuwa ni wao kwa kuwa hayupo tayari kuwa anamtumia fedha zozote.

•Mlalamishi anasema bintiye wa kidato cha pili hajaweza kufungua shule tangu Aprili 26 kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko
Image: Facebook// Mike Sonko

Aliyekuwa gavana wa Nairobi Mike Sonko ameapa kuwa hatatoa hata peni kwa mwanamke ambaye anamshtaki kwa madai ya kutekeleza mtoto wao.

Mwanadada mmoja aliwasilisha kesi mahakamani akimshtumu Sonko kwa kukataa majukumu ya malezi ya binti wa miaka 15 ambaye anadai kuwa alipata naye. 

Mwanadada huyo alitaka mahakama iingilie kati huku akitaka mwanasiasa huyo alazimishwe kumpatia Sh448,450 kila mwezi.

Sonko hata hivyo ameagiza mwanadada huyo amkabidhi mtoto huyo anayedai kuwa ni wao kwa kuwa hayupo tayari kuwa anamtumia fedha zozote.

"Nitampa mtoto huyo kila kitu bora zaidi ambacho dunia inacho. Familia yangu inaendelea kukua siku baada ya siku, ninahisi furaha na kubarikiwa kuwalea watoto yatima, familia za mitaani na watoto waliotelekezwa nyumbani kwangu," Sonko alisema kupitia Facebook.

Kulingana na gavana huyo wa zamani, mwanadada huyo ni mpenda anasa na amepiga hatua hiyo ili  aweze kupata fedha za kuponda raha kila siku.

Sonko pia amedai kuwa mlalamishi ana watoto wengine wawili ambao walichukuliwa na aliyekuwa mpenzi wake kwa kuwa alikuwa anamhadaa.

"Hiyo sehemu ya kutoanishwa pesa alafu anaenda kudunda 24/7 ndio hatutaelewana ata kidogo na sitoi hata bob. Hata mtoto awe si wangu amlete tu kwangu ata saii nitamlea vizuri. Na pia madem wengine mkifeel hamuezi cope up na kulea watoi msiwadhulumu kivyovote, waleteni kwangu nitawalea," Alisema.

Karatasi za mahakama zilizofikia Radio Jambo zilionyesha kuwa mwanadada huyo alitaka Sonko aagizwe kuchanga Sh50,000 za chakula na Shopping, 45,000 za kodi, 30,000 za ulinzi, 20,000 za nguo, 20,000 za mjakazi, Sh20,000 za matibabu, Sh4000 za kutengenezea nywele ya mtoto, Sh5000 za DSTV, 50,000 za karo , Sh5000 za gesi kati ya zingine.

Mwanamke huyo ambaye jina lake limefichwa anasema bintiye wa kidato cha pili hajaweza kufungua shule tangu Aprili 26 kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Anataka mwanasiasa huyo aagizwe kulipa karo ya Sh86,000, Sh30,450  za matumizi mengine ya shule na salio la karo la Sh37,000 huku kesi hiyo ikisubiriwa kuamuliwa. 

Mlalamishi alisema walijitosa kwenye mahusiano mwaka 1999 ambao uliishia kwenye uhusiano wa kimapenzi na kuzaliwa kwa mtoto mnamo April 17, 2007.