Mchuuzi akamatwa kwa kuuza nyama ya mbwa iliyokaangwa Nyandarua

Muhtasari

•Kichwa cha mbwa, sufuria  aliyokuwa akitumia katika mapishi, kisu na panga zilizokuwa na damu, mtego aliotumia kunasa mbwa na gramu 10 za bangi ni baadhi ya vitu vilivyopatikana nyumbani kwa mshukiwa.

Ndirangu Wahome akamatwa kwa kuuza nyama ya mbwa
Ndirangu Wahome akamatwa kwa kuuza nyama ya mbwa
Image: HISANI

Polisi katika kaunti ya Nyandarua wanamzuilia mwanaume mmoja anayeripotiwa kuuzia watu nyama za mbwa.

Ndirangu Wahome alikamatwa Jumapili baada ya chifu wa eneo la Wanjohi, kaunti ndogo ya Kipipiri  Margaret Wambui kuwafahamisha polisi kuhusu mwanamume aliyeshukiwa kuuza nyama ya mbwa iliyokaangwa katika eneo lake.

Wambui alisema kulikuwa na ripoti nyingi zilizodai kuwa nyama ambayo mshukiwa alikuwa akiuza kuzunguka kwenye bakuli katika mji wa Wanjohi mjini Wanjohi ilikuwa ya mbwa.

Baada ya kupokea ripoti polisi walimkamata Ndirangu na kufanya msako mkali nyumbani kwake katika juhudi za kutafuta ushahidi zaidi.

Kichwa cha mbwa, sufuria iliyokuwa ikitumia katika mapishi, kisu na panga zilizokuwa na damu, mtego aliotumia kunasa mbwa na gramu 10 za bangi ni baadhi ya vitu vilivyopatikana nyumbani kwa mshukiwa.

Polisi pia waliweza kumpata mbwa aliye hai ambaye inaaminika alikuwa anasubiri kuchinjwa.

Mshukiwa alitiwa pingu na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Wanjohi ambako anazuiliwa huku akisubiri kufikishwa mahakamani.