Mwili wa mwanafunzi wa Chuo Kikuu wapatikana ukining'inia kwenye kabati ya nguo

Muhtasari

•Mwili wa Nicole Chemutai Serem ulipatikana kwenye kabati lake la nguo ukiwa umefungwa kitambaa shingoni.

• Mkuu wa polisi wa Langata Benjamin Mwanthi alisema bado hawajabaini kilichopelekea kisa hicho.

crime scene
crime scene

Polisi wanachunguza na kisa ambapo mwili wa mwanafunzi wa kike uligunduliwa katika hosteli moja jijini Nairobi.

Mwili wa Nicole Chemutai Serem ulipatikana kwenye kabati lake la nguo ukiwa umefungwa kitambaa shingoni.

Serem 21, ambaye alikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Strathmore, alikuwa katika mwaka wake wa pili.

Msimamizi wa hosteli hiyo alisema alikuwa amekosa kumuona binti huyo kwa muda wa siku mbili na kushangaa alikoenda.

Hapo ndipo alipofungua mlango wa chumba chake na kukuta mwili wake kwenye kabati la nguo.

Polisi waliitwa na kuuchukua mwili huo. Mkuu wa polisi wa Langata Benjamin Mwanthi alisema bado hawajabaini kilichopelekea kisa hicho.

Alisema walikuwa wametoa taarifa kwa familia na kupanga uchunguzi wa mwili wa marehemu.

"Mwili haukuwa na majeraha wakati ulipogunduliwa na hakukuwa na barua ya kujiua. Tunachunguza,” alisema.

Visa vya watu kujitoa uhai vimeendelea kuongezeka nchini huku kukiwa na wito wa kushughulikia hali hiyo.

Kwingineko, polisi wanachunguza kisa ambapo mwanamke mmoja alipatikana amefariki katika baa moja eneo la Kasarani, Nairobi.

Mwanamke huyo aliyetambulishwa kama Njeri tu mwenye umri wa takriban miaka 28 alikuwa ameandamana na wanaume wawili kwenye baa hiyo kabla yao kumuacha akiwa ameketi hapo, walioshuhudia waliambia polisi.

Ilikuwa hadi masaa mengi baadaye ambapo wasimamizi wa hoteli hiyo walipogundua kuwa hakuwa amehama kutoka kwenye kiti chake na walipokagua wakagundua kuwa haitiki.

Mwili huo ulichukuliwa na kupelekwa hadi katika chumba cha kuhifadhia maiti kabla ya zoezi la utambuzi na uchunguzi wa maiti kufanyika. Hakuna aliyekamatwa hadi sasa.

Na polisi wanasaka kundi la waendesha bodaboda waliomdunga mtu hadi kufa katika mabishano katika mitaa ya mabanda ya Mathare, Nairobi.

Mwanamume huyo aliyetambulika kama Morgan Njuguna, 22 alidungwa kisu na kufariki akiwa hospitalini baada ya makabiliano hayo. Walioshuhudia wanasema walikuwa wanabishana kwa sababu zisizojulikana kabla ya kudhoofika kwa mapigano na mauaji ya kisu katika tukio la Jumamosi usiku.

Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti huku msako wa watu wanaoshukiwa kuwa wauaji ukiendelea.