5 wafariki, 12 wajeruhiwa baada ya treni kugonga lori Kiambu

Muhtasari

•Lori husika lilikuwa limesimama kwenye njia ya reli katika eneo la Kihunguro huko Ruiru na kusababisha ajali hiyo.

•Ripoti iliyotolewa na NTSA wiki jana ilionyesha kuwa zaidi ya vifo 1900 vimesababishwa na ajali za barabarani mwaka huu pekee.

Ajali
Ajali
Image: HISANI

Watu watano walipoteza maisha yao katika ajali iliyohusisha treni na lori katika eneo la Ruiru, kaunti ya Kiambu.

Ajali hiyo iliyotokea Jumatatu jioni pia iliacha watu kumi na wawili wakiwa wamejeruhiwa.

Lori husika lilikuwa limesimama kwenye njia ya reli katika eneo la Kihunguro huko Ruiru na kusababisha ajali hiyo.

Mkasa huo unajiri siku moja baada ya watu wengine kumi na wawili kuangamia kwenye ajali ya barabarani katika eneo la Kitui walipokuwa wakielekea kwenye hafla ya mahari.

Inaripotiwa kuwa matatu hiyo ya abiria 14 ilikuwa imebeba kupita kiasi kinachohitajika huku manusura wakimlaumu dereva kwa ajali hiyo.

Manusura waliozungumza na vyombo vya habari walimshutumu dereva huyo kwa kulewa na kuendesha gari vibaya licha ya onyo lao.

Matatu hiyo ilikuwa na watu 24.

Katika ajali nyingine kwenye barabara ya Bomet -Narok, watu 8 walipoteza maisha siku ya Ijumaa baada ya trela kupoteza mwelekeo na kugonga gari la Ena Coach la abiria 14.

Watano walifariki papo hapo huku watatu wakiaga dunia walipokuwa wanapokea matibabu  hospitalini.

Wengine wanne wanaendelea kupokea matibabu katika hospitali ya kaunti ya Narok.

Ripoti iliyotolewa na NTSA wiki jana ilionyesha kuwa zaidi ya vifo 1900 vimesababishwa na ajali za barabarani mwaka huu pekee.