Jamaa aenda mafichoni baada ya kumuua mwanamke - Embakasi

Muhtasari

• Polisi walisema wanamsaka Peter Kamau Kuria mwenye umri wa miaka 32 kuhusiana na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 25.

• Mwanamke huyo alikuwa amemtembelea Kuria nyumbani kwake Alhamisi asubuhi kabla ya mzozo kuzuka kati yao.

Crime Scene

Mwanamume mmoja yuko mafichoni baada ya kudaiwa kusukuma mpenzi wake kutoka orofa ya tano katika eneo la Drive Inn Nairobi.

Polisi walisema wanamsaka Peter Kamau Kuria mwenye umri wa miaka 32 kuhusiana na kifo cha mwanamke mwenye umri wa miaka 25.

Mwanamke huyo alikuwa amemtembelea Kuria nyumbani kwake Alhamisi asubuhi kabla ya mzozo kuzuka kati yao.

Wapangaji wa nyumba hiyo waliwaambia polisi kwamba walisikia kishindo kwenye ghorofa ya chini na walipoangalia, waliona mwili wa mwanamke huyo ukiwa na damu nyingi.

Alikuwa amepasuka fuvu la kichwa na kufa katika eneo la tukio wakati wa kisa cha saa nane usiku.

Polisi waliitwa kwenye eneo la tukio na wakabaini kuwa Kuria hakuwepo nyumbani mwake na ilikuwa imefungwa.

Walinzi katika ghorofa hiyo ni miongoni mwa waliohojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Kamanda wa polisi wa Nairobi James Mugera alisema wanamsaka mshukiwa.

"Hatujui ni nini kilijiri lakini tunamtafuta mshukiwa anayejulikana kwa habari zaidi," alisema Mugera.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi.

Kwingineko, katika mtaa wa Embakasi, mvulana wa umri wa miaka 11 alivunjika taya, mikono yote miwili na mguu wa kulia aliporuka kutoka orofa ya tatu ya shule yao baada ya kuadhibiwa na wasimamizi wa shule hiyo.

Polisi walisema kuwa waliarifiwa mvulana huyo alikuwa hospitalini baada ya kuruka katika jaribio la kujiua kwa kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu.

Polisi walisema wanachunguza tukio hilo.