logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Mwanaume afariki kwa kujitoa uhai baada ya mkewe kumnyima kitambulisho kwa ajili ya mkopo

Marehemu alikuwa amehusika katika visa vingi vya uhalifu.

image
na

Makala15 June 2022 - 04:27

Muhtasari


•David Kipliman alijitoa uhai baada ya mkewe Winnie Mulongo kukataa  ombi lake la kutaka kitambulisho chake kitumike kununua pikipiki kwa mkopo.

•Marehemu alikimbia nyumbani kwake baada ya wanakijiji kumzuia kumchoma kisu mkewe kwa mara ya pili.

Kitanzi

Wakaazi wa mtaa wa Kachibora eneo la Trans Nzoia Mashariki wamekumbwa na mshtuko baada ya mwili wa mwanaume wa miaka 39 kupatikana ukining'inia kwenye paa la nyumba yake kufuatia kutofautiana na mkewe.

Mwanamume huyo aliyetambulika kama David Kipliman Kiprono alijitoa uhai baada ya mkewe Winnie Mulongo Wanyama kukataa  ombi lake la kutaka kitambulisho chake kitumike kununua pikipiki kwa mkopo.

Mzee wa kijiji cha eneo hilo Samuel Kariuki alisema kuwa marehemu alifika nyumbani mwendo wa saa tanu asubuhi na kumpata mkewe na watoto wake wakiwa wamelala kisha kujaribu kuwadunga kisu.

Alisema mke wa marehemu alipiga nduru ambayo iliwavutia majirani waliokimbia pale na kumpokonya mwanamume huyo silaha.

Aliongeza kuwa mwanamume huyo ambaye alionekana kupitia mateso ya kisaikolojia alikasirishwa na hatua ya mkewe kukataa kumpa kitambulisho chake na hivyo kuamua kujaribu kumuua yeye na watoto wake.

“Wanakijiji wa hapa wamethibitisha kuwa kweli wanandoa hao walikuwa na misukosuko iliyojaa kutoelewana mara kwa mara, inasemekana mwanamke ameachwa peke yake na watoto,” alisema.

Mzee huyo wa kijiji alisema marehemu alikimbia nyumbani kwake baada ya wanakijiji kumzuia kumchoma kisu mkewe kwa mara ya pili.

“Alikimbilia nyumbani kwake na ili azuiwe kutoka nje wanakijiji walifunga mlango kutoka nje na kutoa taarifa kwa polisi,” alisema.

Mzee huyo wa kijiji hicho alisema Kipliman alijinyonga kwa kutumia kamba baada ya wakazi kumzuia kutoroka kupitia shimo alilofanikiwa kuchimba kwenye nyumba yake iliyoezekwa na udongo.

Maafisa wa polisi kutoka DCI na matukio walishughulikia eneo la tukio na kuupeleka mwili wa marehemu hadi katika chumba cha kuhifadhi maiti cha hospitali ya rufaa ya Kitale ukisubiri uchunguzi wa maiti.

Afisa wa Upelelezi wa Jinai Kaunti ya Trans Nzoia Francis Kihara alisema kuwa marehemu alikuwa amehusika katika visa vingi vya uhalifu.

Kulingana na picha zilizopatikana katika eneo la uhalifu marehemu alikuwa amehusika katika vitendo kadhaa vya uhalifu.

Alisema uchunguzi umeanzishwa.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved