Makurutu 10 wa polisi katika chuo cha mafunzo ya polisi cha Kiganjo wametiwa mbaroni kwa kughushi stakabadhi zao za elimu.
Kumi hao ambao walikuwa wamejiandikisha kuwa makonstabo wa polisi walikamatwa Jumatano jioni na mafunzo yao kukatizwa mara moja.
Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Baraza la Kitaifa la Mitihani nchini Kenya (KNEC) kuthibitisha kuwa vyeti vya KCSE vya washukiwa sio halali.
"Uchunguzi wa vyeti vyao vya kughushi ulionyesha kuwa baadhi ya madaraja ya somo na wastani yalibadilishwa kimakusudi ili kuendana na mahitaji ya chini kabisa ya kujiunga na huduma ya polisi," Taarifa iliyotolewa na DCI Alhamisi ilisoma.
Vyeti hivyo ghushi vilichukuliwa na kuhifadhiwa kama ushahidi utakaotumika dhidi ya washukiwa mahakamani.
"Washukiwa hao wamepoteza nafasi zao katika huduma ya polisi baada ya kufeli mtihani wa uadilifu na miezi mitatu ya mafunzo makali nyuma ya ua nene wa Kayaba, ambao ni sifa ya chuo cha mafunzo cha polisi cha Kiganjo," Taarifa hiyo ilisoma.
Kumi hao wametambulishwa kama Mochama Opiyo Clive, Muithi John Kitavi, Natembea M. Kelvin, Nyapola Felix Angatia, Mwaulid Galgalo Bide, Gobra Grindguest, Ndambuki Irene Nzisa, Felix Kipkoech Langat, Kabatha Paul Kimani na John Crispus Amisi.
Washukiwa ni miongoni mwa makurutu 5,000 ambao walijiunga na chuo cha Kiganjo mwezi Machi.
Haya yanajiri huku kukiwa na ongezeko la kesi za ughushi wa stakabadhi za elimu nchini hasa miongoni mwa wanasiasa wanaowania nyadhifa za kisiasa.