Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta wakamatwa kwa kudukua akaunti za watu na kuiba pesa

Muhtasari

•Wawili hao walikuwa pamoja na wanawake wawili walipokamatwa katika nyumba yao ya kifahari.

•Inaripotiwa kuwa washukiwa wamekuwa wakiziandamana zaidi akaunti za watu wanaishi nje ya nchi.

Pingu
Image: Radio Jambo

Wapelelezi wa DCI wanawazuilia wanafunzi wawili wa Chuo Kikuu cha Kenyatta kwa madai ya wizi wa pesa kupitia udukuzi wa kadi za benki.

Francis Maina ,26, na Zellic Alusa ,25, walikamatwa Jumatano katika eneo la Mimilani, mjini Nakuru baada ya kuwa kwenye rada za polisi kwa siku kadhaa. Wawili hao walikuwa pamoja na wanawake wawili walipokamatwa katika nyumba yao ya kifahari.

Inaripotiwa kuwa wamekuwa wakidukua kadi za benki za watu kisha kuzitumia kununua bitcoins. Baada ya kununua bitcoins, washukiwa wanadaiwa kuzibadilisha tena kuwa pesa za Kenya kwa ajili ya matumizi.

Kitengo cha DCI kimeripoti kuwa washukiwa wamekuwa wakidukua akaunti za watu kutumia akaunti bandia za barua pepe walizotengeneza.

Inaripotiwa kuwa washukiwa wamekuwa wakiziandamana zaidi akaunti za watu wanaishi nje ya nchi.

Baada ya kufanikiwa washukiwa wanadaiwa kuzitumia hela walizoiba kuishi kifahari, kutumbuiza wanadada na kununua mali.

Pale nyumbani kwa washukiwa polisi waliweza kupata hati za mauzo ya jumba la Ksh850,000 lililo katika eneo la Juja, Kiambu.

Pia walifanikiwa kupata kompyuta tano za mkononi, simu nne, vifaa viwili vya Wi-Fi, kadi kadhaa za simu kati ya vitu vingine.

Usalama wa kidijitali umeboreshwa nchini Kenya baada ya rais Kenyatta kuagiza kuimarishwa kwa maabara ya uchunguzi wa kidijitali.