Miguna awashtaki Matiang'i na Kibicho kufuatia kufurushwa kwake, adai fidia ya Bilioni 1.7

Muhtasari

•Miguna alisema baada ya kukamatwa, alizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka kinyume na Katiba ya Kenya na kuteswa kwa muda wa siku sita.

•Alisema fidia hiyo itagharamia madhara yaliyotokana na kufurushwa kwake.

Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Miguna Miguna afurushwa kutoka Kenya mnamo Machi 2018
Image: MAKTABA

Wakili Miguna Miguna amewasilisha kesi dhidi ya Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i akitaka alipwe fidia ya Sh1.7 bilioni.

Kesi hiyo iliwasilishwa katika Mahakama ya Ontario, nchini Kanada siku ya Alhamisi.

Alisema fidia hiyo itagharamia madhara yaliyotokana na kufurushwa kwake, ambayo ni pamoja na kushambuliwa, kuharibiwa jina na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria miongoni mwa mengine.

Wengine walioshitakiwa katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Karanja Kibicho na makampuni ya kimataifa; Sitel Operating Corporation and Refinitiv Limited. 

Miguna alisema kufurushwa kwake mwezi Februari 2018 kuliharibu sifa yake.

“Mlalamikaji anadai kwa pamoja na kwa kiasi kikubwa fidia ya kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria, mateso, shambulio na kudhulumiwa kwa jumla ya Sh1.1 bilioni na fidia nyingnine ya jumla ya Sh587,050,000 kwa kuharibiwa jna, " hati ya mahakama iliyoonyeshwa na Miguna ilisoma.

Miguna aliiambia Mahakama kuwa alikuwa wakili bora wa Ontario kwa zaidi ya miaka 27, vile vile mwandishi, mtoa maoni, wakili na mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Kenya, na mkazi wa Mkoa wa Ontario.

Wakili huyo anadai zaidi fidia ya Sh234,820,000 kwa ukiukaji wa faragha alioufanya wakati wa kukamatwa kwake nyumbani kwake kabla ya kufukuzwa nchini.

Miguna alisema baada ya kukamatwa, alizuiliwa bila kufunguliwa mashtaka kinyume na Katiba ya Kenya na kuteswa kwa muda wa siku sita.

"Siku ya sita, maajenti wa usalama wa Kenya waliokuwa na silaha nzito chini ya amri ya moja kwa moja ya washtakiwa Matiang'i na Kibicho walimfukuza mlalamikaji kwa nguvu hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (ambao unajulikana kama "JKIA") jijini Nairobi na kumlazimisha kuingia. ndege ya KLM kuelekea Amsterdam," kesi hiyo ilisomeka zaidi.

Pia alisema mara kwa mara, Matiang'i na Kibicho walihutubia wanahabari wakichukua jukumu la kuzuiliwa kwake na kushtakiwa.