Mshukiwa wa ulawiti anayesakwa nchini Uingereza akamatwa nchini Kenya

Muhtasari

Mshukiwa wa kulawiti anayesakwa nchini Uingereza akamatwa nchini Kenya

Image: DCI/TWITTER

Maafisa wa upelelezi wamemkamata mtoro Mkenya ambaye anasakwa nchini Uingereza kwa kosa la kuwadhalilisha watoto kingono.

Anthony Kinuthia Kamau amekuwa mtoro baada ya kuruka dhamana nchini Uingereza.

Mkuu wa DCI George Kinoti alisema alikamatwa na maafisa wa upelelezi katika kitengo cha uhalifu wa kimataifa.

Alisema mshukiwa anahitajika kujibu mashtaka ya unyanyasaji wa kingono kwa watoto katika Mahakama ya Chelmsford ya Uingereza na Ireland Kaskazini.

"Mshukiwa huyo anaripotiwa kuwadhulumu kingono wasichana wa umri wa miaka 11 kuanzia 2005," Kinoti alisema Ijumaa.

Alifichua kuwa Kinuthia alishtakiwa kwa makosa manne ya kujihusisha na ngono isiyo ya kipenyo na msichana mmoja na shtaka lingine la kushawishi msichana mdogo kufanya ngono mnamo Novemba, 2019.

Mshukiwa aliachiliwa kwa dhamana lakini alikimbilia Kenya ambako amekuwa akifanya msako wake kuwa kama mchezo wa paka na panya hadi alipokamatwa Ijumaa.