Kizaazaa baada ya polisi kuzuia mkutano wa Ruto uwanjani Jacaranda

Muhtasari

•Polisi waliwekwa uwanjani huo Jumapili asubuhi na kuwazuia waandalizi kufanya shughuli zozote.

•Polisi walisema walipokea taarifa kuhusu wahuni waliopanga kuvamia mkutano huo na kusababisha madhara 

Image: DP RUTO/TWITTER

Mzozo ulichimbuka kati ya maafisa wa kulinda usalama na kikosi cha Muungano wa Kenya Kwanza Alliance kuhusu mkutano uliopangwa kufanyika katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi.

Hii ilifuatia hatua ya polisi kufutilia mbali mkutano huo kwa kile walichokitaja kuwa sababu za kiusalama.

Polisi waliwekwa uwanjani huo Jumapili asubuhi na kuwazuia waandalizi kufanya shughuli zozote.

Lakini katika kuonyesha kukaidi, Naibu Rais William Ruto ambaye ni mkuu wa Kenya Kwanza aliwaambia wafuasi wake waende uwanjani.

"Washirika wa Kenya Kwanza na Hustler Nation nzima inawatakia Jumapili yenye baraka kwa wote na tukutane Jacaranda baada ya kanisa," Ruto alisemakupitia mitandao ya kijamii.

Haya yallijiri muda mfupi baada ya saa tatu asubuhi alipopata habari kwamba makumi ya maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami walikuwa wamefunga uwanja huo.

Waandalizi wa hafla hiyo hawakuweza kuweka jukwaa ili kuwawezesha kuandaa mkutano huo.

Mkutano huo ulikuwa umetangazwa na miongoni mwa wengine mgombeaji wa ugavana wa Nairobi Johnson Sakaja ambaye sasa anakumbwa na matatizo chungu nzima, ambaye alitaka kuutumia kujipigia debe.

Polisi walisema walipokea taarifa kuhusu wahuni waliopanga kuvamia mkutano huo na kusababisha madhara kwa watu wengi hivyo basi kuchukua hatua ya kuusimamisha.

Maafisa walisema walikuwa wameagizwa kutomruhusu mtu yeyote kufika uwanjani siku ya Jumapili.

“Waje wakipenda lakini wajue mkutano haufanyiki kwa leo. Wanaweza kujaribu kesho,” afisa mmoja mkuu alisema.

Polisi wa kupambana na ghasia walitumwa eneo hilo mwendo wa saa nne asubuhi na kuwazuia yeyote aliyejaribu kuingia.

Wale waliotaka kusimamisha jukwa ili kutumika kama eneo la VIP walikatazwa.

Hili lilileta kumbukumbu za 2017 polisi waliposimamisha mkutano sawia ambao ulipangwa huko na timu ya wakati huo ya Nasa, ambayo iliongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Baadhi ya waliopinga mkutano huo kisha walifikia hatua ya kumwaga kinyesi cha binadamu uwanjani ikiwa ni sehemu ya juhudi za kusitisha mkutano huo.

Wafuasi wa naibu rais, hata hivyo, wameapa kuendelea na mkutano huo.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Paul Ongili almaarufu Babu Owino pia alidai kuwa alikuwa amepanga mkutano wake pale lakini akaghairi Jumapili asubuhi.

Alisema alikuwa na haki kamili ya kutumia uwanja huo lakini alipendelea wafuasi wake wabaki nyumbani.

"Nilikuwa nimeweka eneo la Jacaranda Grounds kwa hafla yangu leo ​na kuwaarifu polisi huku Ruto akipanga eneo hilo hilo siku hiyo hiyo lakini mnamo 2021 kulingana na barua yao ya arifa. Nina haki kamili ya kutumia uwanja huu leo ​​lakini acha Watu wangu wakae nyumbani kwa sababu tunapenda amani,” Babu alisema.

Aidha alisema polisi ambao wamesimama katika uwanja huo walikuwa wakilinda uwanja huo kutoka kwa Ruto ambaye alidai "ana uhusiano mkubwa na Ardhi."

“Hii naye hautagrab. Ninawashauri kwa unyenyekevu watu wangu kutoka Jamhuri ya Embakasi Mashariki kukaa nyumbani au kufanya shughuli zao kwani malaika wa kifo (Ruto) atakuwa akiwatembelea leo,” Babu alisema.