Mwanafunzi taabani baada ya kupatikana na misokoto 16 ya bangi, viberiti shuleni

Muhtasari

•Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19 alinaswa akiwa na roli 16 za bangi wakati wa ukaguzi wa bweni.

•Polisi wamelaani vikali matumizi ya dawa za kulevya shuleni huku wakiwataka wanafunzi wote kujiepusha nazo na badala yake kutia bidii masomoni.

Image: NPS

Polisi katika kaunti ya Migori wanamzuilia mwanafunzi mmoja wa shule ya upili baada ya kupatikana na dawa za kulevya shuleni.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 19 alinaswa akiwa na roli 16 za bangi wakati wa ukaguzi wa bweni uliofanywa katika shule hiyo iliyo eneo la Ntimaru siku ya Jumatatu.

Wasimamizi wa shule pia waliweza kupata mshukiwa akiwa ameficha kiberiti kimoja cha vijiti, kiberiti cha gesi na karatasi mbili za kufungia sigara.

Polisi wameripoti kuwa mshukiwa alikamatwa baada ya wasimamizi wa shule kupiga ripoti kuhusu yaliyojiri.

"Hili linapaswa kutoa onyo kwa wanafunzi wote kuepuka njia ya uhalifu kupitia matumizi mabaya ya dawa za kulevya na aina nyinginezo za uhalifu. Utumiaji wa madawa ya kulevya hauna faida katika maisha, husababisha tu uharibifu," Tume ya Huduma kwa Polisi (NPS) ilionya katika taarifa yake ya Jumanne.

NPS ililaani vikali matumizi ya dawa za kulevya shuleni huku ikiwataka wanafunzi wote kujiepusha nazo na badala yake kutia bidii masomoni.

Haya yanajiri takriban miezi miwili tu baada ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni dhidi ya Unywaji wa Pombe na Madawa ya Kulevya (NACADA) kutoa wito kwa wazazi, shule na washikadau wengine wanaohusika na usimamizi wa taasisi za masomo kusaidia katika vita dhidi ya unywaji pombe na matumizi ya dawa za kulevya shuleni.

"NACADA imekuwa ikitoa mafunzo kwa walimu waliochaguliwa ili kuimarisha zaidi afua za kuzuia na usimamizi shuleni," Taarifa iliyotolewa na NACADA mnamo Mei 15 ilisoma.

Wizara ya Elimu pamoja na mamlaka hiyo iliandaa Miongozo ya Kitaifa ya Kuzuia Matumizi ya Pombe na Madawa ya Kulevya, na Usimamizi katika Vyuo vya Mafunzo ya Msingi ili kusaidia kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya.

Mpango huo unashughulikia uwongo na habari potofu juu ya matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya.

NACADA ilisema kuwa mwongozo huo unatarajiwa kujenga umati wa wafanyakazi na mabalozi wa kupambana na matumizi ya dawa za kulevya ambao wana ujuzi wa kimsingi wa kugundua na kushughulikia matumizi ya dawa za kulevya shuleni.