TSC yakana madai ya kuzuia walimu kuhudumu kama maafisa wa IEBC uchaguzini

Muhtasari

• Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa TSC imewaagiza wakuu wa shule kutowapa walimu ruhusa kuchukua kazi hizo.

• Nafasi zilizotangazwa zilijumuisha maafisa Wasimamizi, Naibu Maafisa Wasimamizi na kazi za ukarani miongoni mwa zingine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kuajiri Walimu Nancy Macharia
Image: ENOS TECHE

Ripoti kuwa Tume ya Kuajiri Walimu nchini TSC imepiga marufuku walimu kuchukua kazi za muda za IEBC ni feki.

Madai yaliibuka yakiashiria kuwa walimu hawataruhusiwa kuchukua kazi za IEBC.

Ripoti hiyo pia ilionyesha kuwa TSC imewaagiza wakuu wa shule kutowapa walimu ruhusa kuchukua kazi hizo.

TSC hata hivyo, amekanusha ripoti hizo na kusema kwamba habari hizo ni za uongo na za kupotosha.

Katika tweet iliyo na picha ya skrini ya ripoti hiyo ghushi, TSC ilisema: " Tume imevutiwa na habari hizi za uongo. Zichukulieni kwa dharau inayostahili".

Ripoti hiyo ya kupotosha ilijiri wakati ambapo IEBC inawaorodhesha watu waliotoa maombi kwa kazi mbalimbali za muda ilizotangaza wiki zilizopita kwa sababu ya kuendesha uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huu.

Nafasi zilizotangazwa zilijumuisha maafisa Wasimamizi, Naibu Maafisa Wasimamizi na kazi za ukarani miongoni mwa zingine.

Duru za kuaminika zimesema kwamba walimu wengi kote nchini ni miongoni mwa waliowekwa kwenye orodha fupi ya mchujo.

Wale walioitwa kwenye mchujo wanashauriwa kuhudhuria kwani hakuna amri ya kuwazuia kuchukua kazi ikiwa watafaulu.