Watu wanne wafariki dunia na wengine 132 kujeruhiwa kwenye ajali ya treni Tanzania

Muhtasari

• Taarifa kutoka TRC zinasema kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa 5 za asubuhi leo ambapo mabehewa nane yaliyokuwa na jumla ya abiria 930 yalianguka katika eneo la Malolo.

Image: Mtandao wa Twitter

Watu wanne wamefariki dunia na wengine 132 kujeruhiwa kwenye ajali ya treni iliyotokea Tabora, Magharibi mwa Tanzania, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limethibitisha.

Taarifa kutoka TRC zinasema kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa 5 za asubuhi leo ambapo mabehewa nane yaliyokuwa na jumla ya abiria 930 yalianguka katika eneo la Malolo.

Katika taarifa hiyo, ilieleza kuwa majeruhi wamefikishwa katika hospitali ya Mkoa ya Kitete kwaaajili ya matibabu huku manusura wakitafutiwa utaratibu wa kumalizia safari zao.

Hata hivyo waliodhibitika ni watoto wawili, mmoja wa kiume na mmoja wa kike. Sambamba na hao wamefariki watu wazima wawili mmoja akiwa ni mwanamke.

Jeshi la Polisi wameeleza kuwa wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajili hiyo.

Matukio ya ajali za treni yametokea mara kadhaa ambapo mwanzoni mwa mwaka huu, treni iliyokuwa ikisafiri Arusha kwenda Dar es Salaam ilipata ajali katika eneo la Pangani, Tanga na kusababisha kifo cha mmoja na majeruhi watano.

Mwaka jana, ajali nyingine ilitokea Bahi- Dodoma ambapo watu watatu walipoteza maisha na wengine 66 kujeruhiwa.

Ikumbukwe mwaka 2002, abiria 280 walipoteza maisha kwenye ajali iliyokea Dodoma.