Polisi ajitoa uhai baada ya kuadhibiwa kwa kulewa akiwa na sare ya kazi

Wenzake marehemu walisema hakufurahishwa na uamuzi wa wakuu wake hivyo akajitoa uhai

Muhtasari

•Mwili wa Konstebo Harrison Mugo ulipatikana ukining'inia kwenye mbao za kantini ya Kituo cha Polisi cha Buruburu.

•Wenzake marehemu walisema hakufurahishwa na uamuzi wa wakuu wake hivyo akachukua hatua ya kujitoa uhai.

Image: HISANI

Hali ya mshtuko ilitanda katika kituo kimoja cha polisi jijini Nairobi wakati mwili wa afisa  ulipopatikana ukining'inia kwenye kantini yao Alhamisi asubuhi.

Mwili wa Konstebo Harrison Mugo ulipatikana ukining'inia kwenye mbao za kantini ya Kituo cha Polisi cha Buruburu.

Alijitia kitanzi katika maandamano ya kupinga hatua za kinidhamu zilizochukuliwa dhidi yake kwa kulewa na kufanya fujo akiwa na sare za polisi.

Wenzake walisema Mugo hakufurahishwa na uamuzi wa wakuu wake hivyo basi akachukua hatua ya kujitoa uhai.

Mwili wake ulikuwa ukining'inia kwenye kamba ulipopatikana na maafisa wengine Alhamisi asubuhi.

Mkuu wa polisi wa Buruburu Kamau Ngugi alisema wanachunguza tukio hilo.

Taarifa kutoka kwa Makao makuu ya polisi iliyoachiwa Jumatano ilisema wamezingatia kipande cha video kinachosambaa kwenye mitandao ya kijamii ambapo afisa wa polisi aliyevalia sare alionekana akitembea peke yake huku akionekana mlevi.

"Hii ni kuuhakikishia umma kuwa tabia hii haifai, haikubaliki na si ya kitaaluma. Huduma ya Kitaifa ya Polisi kwa hivyo inalaani kwa maneno makali iwezekanavyo," msemaji Bruno Shioso alisema.

"Afisa wa polisi aliyevaa sare ni mwakilishi na sura ya serikali inayoonekana na anatakiwa kuwa na nidhamu na weledi wa hali ya juu akiwa kazini na nje ya kazi."

Aliongeza kuwa wakuu wa Polisi katika kituo cha Buruburu walikuwa wamechukua hatua za kurekebisha hali hiyo, na suala hilo linashughulikiwa kwa ndani.

"Kama NPS, tunawawajibisha maafisa wetu kuhusiana na masuala ya nidhamu, adabu, na mwenendo ili kuhakikisha utoaji wa huduma bora kwa umma," alisema.

Wenzake Mugo walisema jambo hilo lilichochea hatua yake kujitoa uhai. Mwili wa marehemu ulihamishwa hadi kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.

Hili ni tukio la hivi punde kutokea na kuathiri huduma. Visa vya kujiua kwa polisi vimeongezeka na wengi wanalaumiwa kwa mfadhaiko na kiwewe kinachohusiana na kazi.

Kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na tatizo hilo, mamlaka zimeanzisha mpango wa ushauri nasaha kwa maafisa hao.

Tume ya Kitaifa ya Huduma ya Polisi ilitangaza kuwa imeanzisha kitengo cha ushauri nasaha ili kutathmini, kubuni, na kuongoza mpango wa kufikia ili kushughulikia matatizo ya afya ya akili na matumizi mabaya ya dawa za kulevya.

Mpango huo pia husaidia familia za polisi na wengine walioathirika na matatizo ya afya ya akili, matumizi mabaya ya dawa za kulevya na kiwewe.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i alisema serikali, NPS na Jeshi la Magereza wameimarisha ushauri na usaidizi wa kimatibabu kwa maafisa.

"Kuna msukumo wa makusudi wa kudharau ugonjwa wa akili na mfadhaiko na kufikia kikamilifu kesi zinazowezekana, ikiwa ni pamoja na kupitia mpango wa Nyumba Kumi," Matiang'i alisema.