Sijaona jina la Ruto kwenye faili ya kesi ya Kimwarer - DPP Haji

Raila alimshutumu Ruto kwa kusitisha ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Muhtasari

•Haji alibainisha kuwa dhana ni kwamba DP anahusishwa na kesi hiyo lakini jina lake halimo kwenye faili zilizoko mahakamani.

• Raila alimshutumu Ruto na washirika wake kwa kusitisha ujenzi wa mabwawa ya mabilioni ya shilingi ya Arror na Kimwarer.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
DPP Norrdin Haji Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji
Image: Maktaba

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji amefichua kuwa hakuna ushahidi wowote ulioletwa dhidi ya Naibu Rais William Ruto kuhusiana na kesi za Arror na Kimwarer.

Akizungumza siku ya Jumatano, Haji alibainisha kuwa dhana ni kwamba DP anahusishwa na kesi hiyo lakini jina lake halimo kwenye faili zilizoko mahakamani.

"Nilinachokijua ni kuwa hakuna ushahidi wowote ulioletwa dhidi yake," alisema.

DPP alisisitiza zaidi kuwa afisi yake haitatumika na watu kupigana kisiasa katika kashfa za mabwawa ya Kimwarer na Arror.

"Hiyo haimaanishi kuwa ninashirikiana na mtu yeyote, ninazungumza ukweli na kusema kwamba jina lake halipo kwenye faili," aliongeza.

Mnamo Novemba 2021, mgombea Urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga alimshutumu Ruto na washirika wake kwa kusitisha ujenzi wa mabwawa ya mabilioni ya shilingi ya Arror na Kimwarer.

Odinga, ambaye alizungumza akiwa ziarani katika Kaunti ya Pokot Magharibi, alisema mabwawa hayo mawili yangekuwa yamekamilika kufikia sasa na kuwahudumia maelfu ya wenyeji katika kaunti za Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet ikiwa si kashfa inayozingira miradi hiyo.

"Serikali ilisema Sh21 bilioni zimeibwa, alafu naibu wa rais anakuja anasema ilikuwa Sh7B” alisema Odinga.

Mwezi Februari 2019, Naibu Rais alikanusha madai kwamba Sh21B zilipotea katika mradi wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer huko Elgeyo-Marakwet akisema ni Sh7B  pekee ndizo zilizohusika.

“Mmesikia kuwa serikali imepoteza Sh21 B katika mabwawa ya Kimwarer na Arror ambayo ni uongo mtupu. Pesa zinazozungumziwa ni takriban Sh7 bilioni na kwa kila sarafu ambayo imelipwa, tuna dhamana ya benki,” Ruto alisema.

Mwezi Novemba mwaka jana, aliyekuwa Waziri wa Hazina Henry Rotich na washtakiwa wenzake walishtakiwa upya katika kashfa hiyo.

Rotich na washtakiwa wenzake walikabiliwa na mashtaka upya baada ya upande wa mashtaka kuomba ruhusa kutoka kwa hakimu wa mahakama Lawrence Mugambi kurekebisha karatasi ya mashtaka ili kuangazia mashtaka mapya.

DPP aliagiza kuondolewa kwa kesi dhidi ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kamau Thuge ili aweze kupatikana kama shahidi wa upande wa mashtaka.

Rotich na washirika wake walishtakiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi na matumizi mabaya ya pesa zilizokusudiwa kwa ujenzi wa mabwawa.

Wote walikanusha malipo katika zabuni za faida kubwa ambazo zilitolewa kwa kampuni ya Italia ambayo wakurugenzi wake bado hawajashtakiwa.

Mnamo Mei 26, 2022 Rotich alishtakiwa upya huku upande wa mashtaka ukiondoa majina ya waliokuwa Makatibu Wakuu Kamau Thugge na Susan Koech ambao walikuwa wameshtakiwa naye.

Wawili hao watatoa ushahidi dhidi ya Rotich wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo.

(Utafsiri: Samuel Maina)