Mwili wa mwanamke aliyeuawa Kisii ungali bado kupatikana

mkono mmoja wa Yunis Bitengo uligunduliwa wakati wa upekuzi kwenye shamba la mahindi

Muhtasari

•Kupotea kwa mwili wa mwanamke huyo kulizua hasira na maandamano siku ya Jumanne baada ya wakaazi kuwashutumu polisi kwa kutochukua hatua.

•Wanafamilia walisema wanataka haki kwa marehemu.

Yunis Bitengo.
Yunis Bitengo.
Image: STAR

Wanakijiji wa Nyakeyo, Mugirango Kusini, wanataka vyombo vya usalama katika eneo hilo kutegua kitendawili kuhusu kifo na kupotea kwa mwili wa nyanya aliyeuawa katika kijiji cha Getonto wiki tatu zilizopita.

Ni mkono pekee wa Yunis Bitengo, alikuwa na umri wa 71, uliogunduliwa wakati wa msako kwenye shamba la mahindi, kilomita moja kutoka nyumbani kwake.

Kupotea  kwa mwili wa mwanamke huyo kulizua hasira na maandamano siku ya Jumanne baada ya wakaazi kuwashutumu polisi kwa kutochukua hatua.

Wanafamilia walisema wanataka haki kwa marehemu.

Wanataka Vigilance House kupeleka wapelelezi wa mauaji ili kusaidia kuwawinda wauaji.

Washukiwa watatu ambao walikuwa wamekamatwa awali wameachiliwa baada ya uchunguzi wa awali kushindwa  kuthibitisha kuwa walihusika na kifo cha huyo mama.

Moses Abuya, mtoto wa Bitengo, alisema mamake alizuru kiwanda cha kutengeneza pombe kwa ajili ya kunywa lakini alishindwa kurejea jambo lililozua wasiwasi.

Baadhi ya vifaa vilivyopatikana katika  eneo la tukio zilikuwa  ni funguo, skafu na wigi alilokuwa amevaa wakati huo alipotoweka.

Omae Nyabuto, mkwe wa marehemu, alisema ingawa suala hilo limeripotiwa kwa polisi huko Etago, uchunguzi bado haujashika kasi.

"Tunataka kuona watu wakikamatwa na mwili kugunduliwa ili kumzika kwa heshima na haki ya haraka," alisema.

Josephat Onderi, jamaa wa familia, alimwomba Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i kusaidia kutegua kitendawili kuhusu kisa hicho.

“Tunamtaka yeye kuhakikisha kuwa  watu wake wamechukua hatua.Inahuzinisha kupoteza mama kwa njia yasiyo eleweka kama hii,” alisema.