Watoto wapatikana wakisafirisha misokoto 347 ya bangi huku mimea 364 iking'olewa

NPS imewakumbusha raia kuwa matumizi ya mihadarati yanaharibu maisha na familia nyingi

Muhtasari

•Polisi waling'oa mimea 364 ya bangi  katika shamba ya mshukiwa ambaye alitambulishwa kama Joseph Ng'ang'a.

•Polisi kutoka Siaya walipata misokoto 347 ya bangi ikiwa imefichwa kwenye suitcase na begi la safari.

Image: NPS

Jamaa mmoja anasakwa na polisi kwa madai ya kupanda bangi katika shamba yake lililoko eneo la Solai, kaunti ya Nakuru.

Jumatano polisi kutoka kituo cha Solai kwa usaidizi wa utawala wa eneo hilo waling'oa mimea 364 ya mihadarati hiyo haramu nchini katika shamba ya mshukiwa ambaye alitambulishwa kama Joseph Ng'ang'a.

Maafisa hao hata hivyo hawakuweza kumtia mbaroni mshukiwa kwani alitoweka na hajulikani aliko hadi kufikia sasa.

Tume ya huduma kwa polisi imetangaza kupitia taarifa kuwa msako dhidi ya mshukiwa umeimarishwa.

Katika tukio tofauti, polisi kutoka kituo cha Unguja, kaunti ya Siaya  waliweza kupata misokoto 347 ya bangi ikiwa imefichwa kwenye suitcase na begi la safari la washukiwa ambao walikuwa wamepanga safari ya kwenda Nairobi.

Washukiwa ambao wanaaminika kuwa watoto wadogo waliacha mizigo yao na kutoweka walipohojiwa na wafanyikazi wa kampuni ya basi ambalo walikuwa wamepanga kuhusu walichokuwa wamebeba.

Polisi wametangaza kwamba uchunguzi unaendelea ili kuwatambua washukiwa na wenye mihadarati ile.

"Tume ya Huduma kwa Polisi, kupitia Idara ya Watoto na Jinsia kote nchini, daima imekuwa ikitetea haki na ustawi wa watoto. Tunawakumbusha umma, hasa wazazi, jukumu lao katika kuwalinda watoto dhidi ya aina yoyote ya ulanguzi na unyanyasaji wa dawa za kulevya kama inavyopendekezwa na Sheria ya Watoto Nambari. 8 ya 2001. Usafirishaji wa bangi ni kosa kubwa na huvutia adhabu kubwa," Taarifa ya NPS imesoma.

NPS pia imewakumbusha raia kuwa matumizi ya mihadarati yanaharibu maisha hasa ya vijana na kuwazuia kuishi maisha mazuri.